CARACAS, Venezuela
KWA sasa, Alejandro Betancourt anatarajiwa kama mtu muhimu katika mkataba wa mafuta ulioingiwa kati ya nchi yake ya Venezuela na Marekani, kwa mujibu wa Rais Donald Trump.
Katika mkataba huo, ambao Trump anauita wa kihistoria duniani, Marekani inatarajiwa kuchota asilimia 20, sawa na mapipa bilioni 65 ya mafuta ghafi ya Venezuela, anaeleza Thomas Posado, ambaye ni mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Rouen.
Kwa upande wake, Rais wa Mpito wa Venezuela, Delcy Rodriguez, amesema mkataba huo wa mia 25 utaingiza Dola bilioni 100 kwenye eneo la uwekezaji nchini kwake.
Hata hivyo, wengi wanatilia shaka uwepo wa milionea wa Venezuela, Betancourt, kwenye mkataba huo, ambapo atakuwa ‘mtu wa kati’ anayeziunganisha Marekani na Serikali ya Venezuela.
Vyombo vya habari vingi, likiwamo jarida la Financial Times, linamtaja tajiri huyo mwenye umri wa miaka 46 kama kibaraka wa Trump nchini Venezuela.
Betancourt, kwa wasiomfahamu, ni kiongozi wa kampuni kubwa ya uzalishaji wa mafuta ya North American Blue Energy Partners (NABEP), ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini Venezuela.
Trump amekuwa akimsapoti Betancourt akisema mfanyabiashara huyo ni kiungo muhimu katika sekta ya mafuta na anaaminiwa na Rais wa Mpito, Delcy.
Delcy amekuwa akimtumia mara kadhaa pia kama mshauri wake wa namna ya kuinua uchumi wa Venezuela, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani na nje ya Venezuela.
Hata hivyo, kwa wananchi wa Venezuela, Betancourt si mtu safi. Tajiri huyo amewahi kukamatwa mara mbili nchini Uingereza, ambako ndiko anakoishi kwa miaka mingi.
Mara ya kwanza ilikuwa Septemba, 2025, ambapo alikamatwa kwa ombi la mamlaka za Hispania, ambazo zilimshutumu kwa utatakishaji fedha na ukwepaji wa kodi lakini aliachiwa kwa dhamana.
Miezi mwili baadaye, Betancourt alikamatwa tena, safari hii akiwa kwenye makazi yake ghali jijini London, akikabiliwa na tuhuma za ubadhirifu na utakatishaji fedha.
Hivyo, kwa shutuma hizo, wanasiasa wa upinzani nchini Venezuela hawaoni kama imekaa sawa kwa tajiri huyo kuchaguliwa kuwa kiungo katika mkataba wao na Marekani, kwa mujibu wa Gazeti la New York Times.
Kwa wananchi wengi wa Venezuela, utajiri wa Betancourt hautokani na jitihada au mipango ya Mungu, bali ujanjaujanja na kupendelewa na Serikali zilizopta chini ya marais Hugo Chavez na Nicolas Maduro.
Mathalan, mwanzoni mwa miaka ya 2010, licha ya kampuni yake ya umeme ya Derwick Associates kutokuwa na uzoefu, alipewa mikataba 11 na serikali, kwa mujibu wa Gazeti la El Pais la Hispania.


