Na Mwandishi wetu, Gazetini
MKUU wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amefichua historia ya urafiki wake wa muda mrefu na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, akisema maisha ya mwanadamu yana mambo mengi yasiyotabirika na kesho ya mtu inajulikana na Mungu pekee.
Mtaka ametoa ujumbe huo kupitia ukurasa wake wa Facebook, siku moja baada ya Ndejembi kuapishwa rasmi kuwa Makamu wa Rais, akirejea picha ya mwaka 2014 iliyopigwa wakati wa harusi yake katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kigurunyembe, Morogoro. Wakati huo Mtaka alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, huku Ndejembi akiwa akifanya kazi katika kampuni ya simu ya Tigo, kabla ya kuhamia Smiles.
Katika simulizi hiyo, Mtaka amesema licha ya kuwa na marafiki wengi waliokuwa viongozi wenzake, aliamua kuwa wasindikizaji wake wa harusi wangekuwa watu aliokuwa na urafiki nao kama Anthony Mtaka, si kwa sababu ya vyeo walivyokuwa navyo. Miongoni mwa waliokuwa katika picha hiyo ni Ndejembi, ambaye sasa ni Makamu wa Rais, pamoja na viongozi wengine ambao wakati huo walikuwa katika nafasi tofauti na walizonazo sasa.
Mtaka amesema katika safari yao ya maisha, yeye na marafiki zake wameendelea kusaidiana na kutiana moyo katika nyakati za furaha, changamoto na vipindi vigumu, akisema kila mmoja amekuwa daraja la ushauri kwa mwenzake.
Akizungumzia Ndejembi, Mtaka amemtaja kuwa mtu mshirikishaji, mnyenyekevu na muungwana, ambaye, kwa mujibu wake, si mtu wa kuwawekea wengine “miba” wala kuwakwaza. Ameongeza kuwa Ndejembi ni mtu anayesikiliza kwa makini, huku akisema “masikio yake yanasikia sana lakini kinywa chake kinaongea kidogo.”
Mtaka amempongeza Ndejembi kwa nafasi hiyo mpya na kumuombea hekima na uongozi mwema katika kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
“Namuombea utumishi mwema, daima hekima ya Mungu imfunze na kumtunza anapomsaidia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku,” amesema Mtaka.


