Na Malima Lubasha, Gazetini
WADAU mbalimbali wa maendeleo pamoja na taasisi wilayani Serengeti, mkoani Mara, wametakiwa kuwawezesha wanawake wajasiriamali wanaofanya biashara katika Soko Kuu la Serengeti kwa kuwasaidia kupata chumba cha baridi kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa zao na kupunguza uharibifu.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mary Surati, Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyayo Foundation ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Serengeti, wakati wa uzinduzi wa hafla ya Samia Uthubutu Awards 2026 iliyowakutanisha vijana wa shule za sekondari kutoka wilaya za Serengeti na Tarime kuonesha vipaji na ubunifu wao. Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Right to Play.
Surati amesema wanawake wengi wanaofanya biashara ya mboga mboga, nyanya, samaki, vitunguu na bidhaa nyingine katika soko hilo, pamoja na kusambaza bidhaa katika maeneo mbalimbali ikiwemo hoteli za kitalii ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa sehemu bora za kuhifadhia bidhaa.
Amesema upatikanaji wa vyumba vya baridi utawasaidia kuhifadhi bidhaa zao katika mazingira salama na kupunguza hasara inayotokana na kuharibika kwa bidhaa.
“Ni muhimu wadau mbalimbali kuwashika mkono na kuwasaidia kupata vifaa vya kuhifadhi bidhaa ili ziweze kudumu na kuwafikia wananchi zikiwa katika ubora unaohitajika,” amesema Surati.
Aidha, Surati amewataka wanawake hao, watakapopata vyumba hivyo, kuhakikisha wanahifadhi bidhaa bora na salama kwa matumizi ya wananchi.
Amesema Nyayo Foundation, iliyoanzishwa Aprili 2025, inalenga kuwawezesha vijana kubuni vitu mbalimbali na kuanzisha miradi ya kiuchumi, huku wanawake wakijengewa uwezo wa kujikwamua kiuchumi, kuongeza kipato na kukuza biashara zao.
Kwa upande wake, Mratibu wa Samia Uthubutu Awards 2026, Modester Michael kutoka Nyasa Foundation, amesema kaulimbiu ya “Ubunifu wa Vijana, Nguvu Kazi ya Tanzania” inalenga kukuza vipaji na ubunifu wa wanafunzi na kuwajengea uwezo wa kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Serengeti, Mrobanda Japan, amepongeza hatua ya kuanzishwa kwa mpango huo, akisema unawapa vijana, hususan wasichana, nafasi ya kuonesha vipaji na ubunifu wao.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayubu Makuruma, amewataka wanafunzi kupenda masomo ya sayansi ili waweze kukuza vipaji na ubunifu wao na hatimaye kuwa wabunifu na wanasayansi bora.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Grumeti Fund, Frida Molell, amesema taasisi hiyo inajihusisha na uhifadhi wa wanyamapori, huduma kwa jamii, mafunzo ya ujasiriamali, utalii, ufadhili wa elimu ya juu na ufugaji wa kisasa. Amewataka wanafunzi kuendelea kuwa wabunifu na kuzingatia masomo ya sayansi.
Akifunga hafla hiyo, Mkuu wa Idara ya Utalii wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Alex Choya, amewataka vijana kutumia uwezo wao kubuni na kutatua changamoto zinazowazunguka ili vipaji vyao viweze kuwa chanzo cha fursa na maisha bora.
Choya pia ameisihi Nyayo Foundation kuendelea kuwajengea uwezo vijana katika kukuza vipaji na ubunifu, huku akiwataka wazazi na walezi kuwaunga mkono watoto wao katika kuendeleza vipaji na ubunifu.
Katika hafla hiyo, tuzo mbalimbali zilitolewa kwa shule zilizofanya vizuri. Makundusi Sekondari ilishika nafasi ya kwanza na kupata Sh milioni moja pamoja na fursa ya kutembelea Bunge, huku Sedeco Sekondari ikishika nafasi ya pili na kupata Sh 800,000 pamoja na ziara ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Matongo Sekondari ya Tarime ilishika nafasi ya tatu na kupata Sh 500,000.


