20.7 C
New York

Kriketi ilivyolificha soka nchini India

Published:

NEW DELHI, India

INDIA ni Taifa lenye watu bilioni 1.45 lakini nafasi yake kwenye viwango vya ubora wa soka vya FIFA ni 138. Mchezo huo uko mahututi nchini humo.

Kriketi ndiyo mchezo ulioshika kasi, huku soka likichezwa kwa kiwango cha kawaida katika majimbo machache ya West Bengal, Goa, Kerala, Mizoram na Manipur.

Wakati huu timu ya soka ya Taifa ya India ikiwa haijafuzu michuano ya Asia ya mwakani (2027), ni ngumu pia kufikiria uwezekano wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2030 na hata zile za 2034.

Zipo sababu nyingi zinazotajwa kuikwamisha India linapokuja suala la mchezo wa kandanda. Moja ya hizo ni kukosekana kwa mfumo bora wa soka la vijana.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka la India (AIFF), Lalnghinglova Hmar, anasema kama kuna eneo linalohitaji nguvu kubwa, basi ni hilo.

“Ukienda Korea Kusini na Japan, timu za watoto zinapata mechi za ushindani zaidi ya 40 kwa msimu mmoja. Hilo hatuna hapa India.

“Tunaanza kuendeleza wachezaji tukiwa tumechelewa sana. Wachezaji wengi wa U-15 wanacheza mechi za ushindani 12 hadi 15 tu kwa mwaka. Wengine wanaitwa timu za taifa (za vijana) wakiwa na mechi zisizozidi 20,” anasisitiza Hmar.

Katika hatua nyingine, Hmar anasema uhaba wa makocha wenye vigezo ni changamoto nyingine kubwa inayolikumba soka la India.

“Tuna uhaba wa makocha bora. Katika baadhi ya majimbo, hakuna hata Ligi za vijana … Hatuwezi kuwa washindani kwa mtindo huo,” anasisitiza.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya soka ya Goa inayoshiriki Ligi Kuu, Ravi Puskur, anasema inahitaji muda kwa soka kufikia mafanikio ya kriketi nchini India.

“Kama utaniuliza, nitakwambia inahitaji miaka minne au zaidi kubadili mfumo uliopo na kuweka mwingine. Hivyo, tutahitaji miaka 20 hadi 25 kufuzu Kombe la Dunia,” amesema.

Aidha, wapo wanaoamini kuwa ongezeko la idadi ya timu zinazoshiriki Kombe la Dunia, ambapo zilifikia 48 mwaka huu, ni ‘tobo’ kwa nchi zenye msuli mdogo wa ushindani wa soka kama ilivyo India.

Related articles

Recent articles