Na mwandishi wetu, Gazetini
UTAFITI wa Shirika la Takwimu za Kazi la Marekani umefichua namna watu nchini humo wanavyozitumia siku zao mbili za mapumziko ya wiki (wikiendi), kwa maana ya Jumamosi na Jumapili.
Lengo la utafiti huo ni kuona watu wanatumia muda mwingi kufanya nini wikiendi, ikilinganishwa na siku za kazi, yaani Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi na Ijumaa.
Ndipo Shirika la Takwimu za Kazi la Marekani lilipobaini kuwa watu nchini humo hutumia wastani wa saa 10 na dakika 26 kulala wikiendi, ikilinganishwa na saa 9 na dakika 26 kwa kwa siku za kazi.
Pia, utafiti ukaeleza kuwa ni watu nchini humo hutumia wastani wa saa 6 na dakika 29 kwa ajili ya burudani na michezo wikiendi, tofauti na saa 4 na dakika 36 kwa siku za kawaida.
Vilevile, wikiendi imeonekana kuwa ‘bize’ kwa shughuli za nyumbani, ikiwamo kufua na kufanya usafi, ambazo hutumia wastani wa saa 2.26, ikilinganishwa na saa 1.88 katika siku nyingine.
Kwa upande mwingine, muda wa kutazama televisheni kwa wikiendi ni wastani wa saa 3.27, tofauti na saa 2.33 kwa siku za kazi.
Kuwa karibu na marafiki na ndugu au kuwasiliana nao kwa njia zingine, ikiwamo simu, nayo imeonekana kuwa na nafasi yake katika siku za wikiendi.
Kwa mujibu wa utafiti huo, watu nchini Marekani hutumia wastani wa saa 1 na dakika 5 katika eneo hilo kwa wikiendi, tofauti na dakika 44 kwa siku za kawaida.
Kwamba ni wastani wa saa 1 na dakika 7 pekee zinazotumika wikiendi kwa ajili ya masuala yanayohusu kazi zao.
Vilevile, masuala yanayohusu dini kwa wikiendi huchukua wastani wa dakika 27 pekee, ikilinganishwa na dakika 13 katika siku za kazi.


