Na mwandishi wetu, Gazetini
MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amekipongeza Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kuendelea kuandika na kuibua changamoto za uharibifu wa mazingira, akisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Msando amesema JET ina nafasi muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu athari za shughuli za binadamu kwa mazingira, hususan uharibifu wa vyanzo vya mito unaoweza kuhatarisha upatikanaji wa maji na kuongeza athari za ukame na uchafuzi.
Ametoa kauli hiyo Agosti 6, 2026, wakati akifungua Jukwaa la Mkutano wa Taasisi Zisizo za Kiserikali (NGOs) Wilaya ya Ubungo, lililobeba kaulimbiu “Fikra Mpya kuhusu Uendeshaji wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kupitia Vyanzo vya Ndani.”

Msando ameitaka JET kuendelea kutumia uandishi wa habari kama nyenzo ya kuhamasisha jamii kuhifadhi vyanzo vya maji, kupanda miti na kuepuka shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira katika maeneo ya mito na vyanzo vyake.
Amesema taarifa za mazingira zinazotolewa kwa wakati zinaweza kusaidia jamii kutambua madhara ya shughuli kama ukataji miti, ufugaji na kilimo kinachofanyika katika maeneo yasiyofaa, huku zikiwezesha mamlaka kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji wa sheria za mazingira.
“JET ina jukumu muhimu la kuelimisha jamii na kulinda rasilimali zetu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Msando.
Ameongeza kuwa uandishi unaolenga vyanzo vya maji unapaswa kwenda sambamba na kuonyesha suluhisho, ikiwemo matumizi ya mbinu bora za kilimo, upandaji miti na uhifadhi wa maeneo yanayozunguka mito.
JET yaweka mkazo vyanzo vya mito
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, amesema taasisi hiyo imeamua kuongeza msisitizo katika uandishi kuhusu vyanzo vya mito vilivyopo Ubungo na maeneo mengine kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii na kuchochea hatua za uhifadhi.
Amesema uandishi huo utalenga kuonyesha namna shughuli za binadamu zinavyoathiri mito na vyanzo vyake, huku ukitoa elimu kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa na jamii na mamlaka kuzuia uharibifu.
Kwa mujibu wa Chikomo, habari za mazingira zinapaswa pia kuelimisha umma kuhusu sheria zinazolinda vyanzo vya maji na athari za kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Amesema JET itaendelea kuangazia shughuli kama ukataji miti, ufugaji na kilimo katika maeneo ya vyanzo vya maji, pamoja na kuonyesha suluhisho zinazoweza kutumika katika kukabiliana na changamoto hizo.
NGO zatakiwa kutafuta suluhu
Katika mkutano huo, Msando amezitaka NGOs zinazofanya kazi katika Wilaya ya Ubungo kuongeza ubunifu, kuimarisha ushirikiano na kutumia fursa za ndani za rasilimali ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema mashirika yanayofanya kazi katika sekta za afya, elimu, mazingira, uwezeshaji wa kiuchumi na kupambana na ukatili wa kijinsia yanapaswa kutumia fursa zilizopo ndani ya jamii kubuni suluhisho endelevu kwa changamoto zinazowakabili wananchi.
Washiriki pia wamejadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mashirika kwa mwaka 2025, ikiwemo mafanikio, changamoto na mipango ya kipindi kijacho.

Mratibu na Msajili Msaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), Wilaya ya Ubungo.
Aidha, Msando amezitaka NGOs ambazo bado hazijakamilisha taratibu za usajili na kupata vibali kufanya hivyo kwa wakati na kuzingatia sheria.
Amehimiza pia Chama cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania (NACONGO) kutumia ofisi za kata kama vituo vya kuratibu shughuli zake ili kuongeza ukaribu na jamii.
Msando amesema NGOs zinapaswa kubuni miradi na fursa za kiuchumi zitakazowasaidia kujitegemea kifedha na kupunguza utegemezi wa wafadhili wa nje.


