30.9 C
New York

Serikali yatoa Sh milioni 400 kwa vijana Ludewa

Published:

Na mwandishi wetu, Ludewa

SERIKALI imetoa mkopo usio na riba wenye thamani ya Shilingi milioni 400 kwa vijana 117 kutoka vikundi vinne vya Kata ya Lupingu, Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, kwa lengo la kuwawezesha kupanua shughuli za ufugaji wa samaki wa vizimba katika Ziwa Nyasa.

Mkopo huo umetolewa kupitia mpango wa kuwawezesha vijana kiuchumi, ukiwa na dhamira ya kuongeza ajira, kuinua kipato na kuchochea maendeleo ya uchumi kupitia miradi ya uzalishaji.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mfano wa hundi za mkopo huo na kutembelea miradi ya wanufaika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema Serikali itaendelea kuwaunga mkono vijana wenye miradi yenye tija ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa.

“Serikali imejipanga kuhakikisha vijana wanapata fursa za mitaji ili waweze kuendeleza shughuli za uzalishaji. Ni muhimu mkopo huu ukatumike kwa malengo yaliyokusudiwa na miradi hii iwe endelevu kwa manufaa ya wanufaika na jamii kwa ujumla,” amesema Nanauka.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Ludewa, Imani Mwaisango, alisema vikundi hivyo vilistahili kupatiwa mkopo huo baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa, ikiwemo kuonyesha uwezo wa kusimamia miradi ya uzalishaji na kuhakikisha inakuwa endelevu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kwa kutumia fursa ya rasilimali zilizopo, hususan Ziwa Nyasa, kuanzisha miradi ya kiuchumi inayowainua vijana na kuwajengea uwezo wa kujitegemea.

Amesema miradi ya ufugaji wa samaki wa vizimba ina mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa samaki, kuimarisha usalama wa chakula, kuzalisha ajira na kukuza uchumi wa wananchi wa eneo hilo pamoja na Taifa kwa ujumla.

Related articles

Recent articles