Na mwandishi wetu, Gazetini
GAZETINI Communication, kupitia chombo chake cha habari cha Gazetini, imeingia makubaliano ya ushirikiano na International Women’s Peace Group (IWPG) ya Korea Kusini yatakayolenga kuimarisha elimu ya amani, uwezeshaji wa wanawake na vijana, pamoja na matumizi ya vyombo vya habari katika kujenga utamaduni wa amani nchini Tanzania.
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi wa IWPG Global Region 2, Seo Yeon Lee, na Mkuu wa Uendeshaji wa Gazetini, iliyo chini ya Gazetini Communication, Faraja Mulungu, ikiwa ni sehemu ya ziara ya IWPG nchini Tanzania iliyofanyika kuanzia Julai 5 hadi 9, 2026.
Kupitia ushirikiano huo, pande hizo zitashirikiana katika kutekeleza programu za Women’s Peace Education (Elimu ya Amani kwa Wanawake), elimu ya amani kwa vijana, kampeni za uhamasishaji wa jamii kuhusu amani, uwezeshaji wa wanawake, pamoja na ushirikiano wa kimkakati wa vyombo vya habari katika kuhamasisha utamaduni wa amani.
Makubaliano hayo yalifikiwa sambamba na shughuli mbalimbali zilizoratibiwa na IWPG nchini Tanzania, zikiwemo mashindano ya kimataifa ya watoto ya International Loving-Peace Art Competition, Jukwaa la Wanawake la Amani Tanzania (Tanzania Women’s Peace Forum), utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano na taasisi mbalimbali pamoja na mazungumzo ya kisera na Serikali.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa IWPG Global Region 2, Seo Yeon Lee, alisema amani haiwezi kujengwa kwa siku moja bali huanza kupitia elimu na ushirikiano wa jamii.

“Amani haiji yenyewe. Amani huanza na elimu. Wanawake si watu wanaosubiri amani, bali ni viongozi wanaoijenga. Ushirikiano huu si kusaini makubaliano pekee, bali ni ahadi ya pamoja ya kujenga amani kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.
Ameongeza kuwa IWPG itaendelea kushirikiana na wanawake, watoto, vijana na taasisi mbalimbali nchini Tanzania ili kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa amani katika familia na jamii zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Uendeshaji wa Gazetini, Faraja Mulungu, amesema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya sekta ya habari na taasisi za kimataifa katika kuhamasisha amani na maendeleo endelevu.
Amesema Gazetini itaendelea kutumia majukwaa yake ya habari kutoa elimu kwa umma kuhusu amani, mshikamano, usawa wa kijinsia na utatuzi wa migogoro kwa njia za mazungumzo, huku ikitoa nafasi kwa wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii salama.
Katika ziara hiyo, IWPG kwa kushirikiana na African Women Leaders Network (AWLN) Tanzania Chapter iliandaa Jukwaa la Wanawake la Amani Tanzania chini ya kaulimbiu “Advancing Peace, Wellness, and Collaboration for Women in Tanzania and South Korea.” Jukwaa hilo lilijadili nafasi ya wanawake katika kujenga amani, ustawi wa jamii na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Korea Kusini.
Mbali na Gazetini Communication, IWPG pia ilisaini makubaliano ya ushirikiano na Tanzania Child Welfare (TCW) ili kupanua utekelezaji wa programu za elimu ya amani kwa wanawake na vijana.
Ujumbe wa IWPG pia ulifanya mazungumzo ya kisera kwa njia ya mtandao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Maswi, ambapo pande hizo zilikubaliana kuendeleza ushirikiano katika elimu ya amani, mashindano ya International Loving-Peace Art Competition, pamoja na programu za kujenga amani katika jamii kupitia ushirikiano wa Serikali na taasisi zisizo za kiserikali.
Ziara ya IWPG nchini Tanzania ilikuwa sehemu ya mpango wake wa kuimarisha mtandao wa ushirikiano wa amani Afrika Mashariki, unaozihusisha serikali, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia, taasisi za elimu na vyombo vya habari, kwa lengo la kujenga utamaduni endelevu wa amani kupitia elimu na ushirikiano wa kimataifa.



