Na Malima Lubasha, Serengeti
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali imeanza mchakato wa kufuta sheria inayoruhusu kutaifishwa kwa mifugo inayokamatwa ndani ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori, baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuelekeza kuwa marekebisho hayo yafanyike katika mkutano wa Bunge wa Agosti mwaka huu.
Dk. Nchemba alitoa kauli hiyo Julai 2, 2026, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Sokoine, Mugumu, wilayani Serengeti mkoani Mara.
Alisema Serikali imebaini kuwa sheria hiyo imekuwa na athari kubwa kwa wananchi, hususan wafugaji, kwa kuwa imechangia baadhi yao kupoteza mali, kufilisika, kuingia katika umasikini na kudhoofisha ustawi wa familia zinazotegemea mifugo kama chanzo kikuu cha uchumi.
“Tunakwenda kuifuta sheria hiyo. Lengo ni kuhakikisha tunapata njia bora zaidi za kushughulikia migogoro kati ya shughuli za ufugaji na uhifadhi bila kuwaadhibu wananchi kwa adhabu zinazowanyang’anya mali zao zote,” alisema Dk. Nchemba.
Alieleza kuwa baada ya sheria hiyo kufutwa, Serikali itaweka utaratibu mwingine utakaosaidia kulinda maeneo ya hifadhi huku ukiendelea kuheshimu haki za wananchi na kulinda maisha yao ya kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Bunge katika mkutano wake uliopita lilipitisha marekebisho ya sheria yatakayowezesha miradi ya ujenzi wa barabara ambayo ilikuwa inasuasua kutokana na ucheleweshaji wa fedha kukamilishwa kwa wakati.
Alisema hatua hiyo itahakikisha fedha za miradi ya miundombinu zinapatikana kwa wakati, hivyo kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini, ikiwemo katika Mkoa wa Mara.
Dk. Nchemba alitaja baadhi ya barabara zitakazonufaika na utaratibu huo kuwa ni barabara ya Mugumu–Tarime na Sanzate–Natta, ambazo ni muhimu katika kuchochea shughuli za kiuchumi na kurahisisha usafiri wa wananchi.
“Hatutakuwa na ucheleweshaji wa fedha katika miradi hii. Tunataka wananchi wa Mkoa wa Mara wapate miundombinu bora itakayowarahisishia shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa mazao na bidhaa nyingine,” amesema.
Waziri Mkuu yuko mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya siku tano inayolenga kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo, pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.


