36.8 C
New York

LeBron kutua wapi msimu ujao NBA?

Published:

LOS ANGELES, Marekani

NI rasmi kwamba supastaa wa Ligi Kuu ya mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA), LeBron James, hatakuwa na kikosi cha Los Angeles Lakers msimu ujao wa 2026-27.

LeBron ni miongoni mwa nyota wenye heshima kubwa NBA, ikiwa ni pamoja na kutwaa mara nne taji hilo, tuzo nne za Mchezaji Bora wa Mwaka (MVP) na zingine nne za Mchezaji Bora wa Fainali.

Msimu uliomalizika, 2025-26, akiwa silaha muhimu ya eneo la ushambuliajia Lakers, alikuwa na wastani wa kufunga pointi 21 na kutoa ‘asisti’ saba katika kila mechi.

Ni miaka nane sasa tangu alipojiunga na Lakers mwaka 2018 na msimu ujao utakuwa wa 24 kwake akiwa NBA.

Baada ya staa huyo mwenye umri wa miaka 41 kusema ataondoka, klabu ya Lakers nayo imethibitisha kwa taarifa ya kumuaga.

“LeBron James ni mmoja ya wachezaji bora katika historia. Tutaendelea kumshukuru kwa miaka yake nane akiwa Lakers, ukiwamo ubingwa aliotupa katika mazingira magumu mwaka 2020.

“Tunamtakia kila la kheri huko mbeleni, ndani na nje ya uwanja. Ataendelea kuwa sehemu ya familia ya Lakers,” imeeleza taarifa ya Lakers.

REKODI ZA KUTISHA

Kwa wachezaji waliopo sasa, LeBron ndiye mwenye umri mkubwa zaidi. Atatimiza miaka 42 ifikapo Desemba, 2026.

Pia, ndiye mchezaji wa kwanza katika historia ya NBA kucheza kwa misimu 23, tena akiwa kwenye bora.

Vilevile, LeBron ndiye mchezaji pekee katika historia ya Ligi hiyo kucheza timu moja na mtoto wake. ‘Dogo’ anaitwa Bronny na anacheza Lakers.

ATATUA WAPI?

Dirisha la usajili kwa wachezaji huru (waliomaliza mikataba na klabu zao) lilifunguliwa juzi Juni 30, 2026.

Baada ya kuthibitisha kuwa ataondoka Lakers, LeBron ameweka wazi kwamba ndoto yake ni kuendelea kutwaa mataji ya Ligi Kuu hiyo.

Golden State Warriors na San Antonio Spurs ya Victor Wembanyama zinatajwa kuitaka huduma yake, kama ilivyo kwa Cleveland Cavaliers na Miami alizowahi kucheza.

Kwa upande wa Golden State, Lebron alikutana nayo mara nne katika mechi za fainali akiwa mchezaji wa Cleveland.

Pia, mkali huyo ana uhusiano mzuri na staa wa Golden State, Stephen Curry, na hata kocha wa timu hiyo, Steve Kerr.

LeBron aliwahi kufanya nao kazi kwenye timu ya Taifa ya Marekani iliyotwaa ubingwa wa Olimpiki mwaka 2024 jijini Paris, Ufaransa.

Ukija kwa Cleveland, alicheza miaka saba ya mwanzoni mwa maisha yake NBA, kabla ya kuhamia Miami, ambako alitwaa mataji mawili ya NBA.

Alipoondoka Miami, alirejea Cleveland na kucheza kwa miaka minne, kabla ya kujiunga na Lakers mwaka 2018.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za NBA, LeBron hatosaini mkataba na klabu yoyote hadi Julai 6, 2026.

Related articles

Recent articles