NEW YORK, Marekani
MWANAUME mmoja amejiua kwa kujichoma moto nje ya Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York.
Kwa upande wao, wanaharakati wamemtaja mtu huyo kwa jina la Lobga Rangzen, wakisema anatokea jamii ya Tibet nchini China.
Kwa mujibu wa taarifa, Rangzen amejiua nje ya UN ili kufikisha ujumbe wa kutaka Tibet ipewe uhuru wake na mamlaka za China.
Inaelezwa kuwa dereva huyo wa ‘Uber’ alifika nje ya ofisi za UN akiwa na bendera ya Tibet, kabla ya uamuzi wake wa kujichoma moto.
Polisi wa New York wamedai kuwa mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 52 alipata majeraha makubwa na kukimbizwa hospitali, ambako alibainika kuwa ameshafariki.
Aidha, taarifa ya polisi imeeleza kwamba bado uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha tukio hilo.


