Na Mwandishi wetu, Gazetini
MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, ametoa siku 90 kwa vikundi vyote vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10 kutoka halmashauri mbalimbali mkoani humo ambavyo bado havijarejesha fedha hizo kuhakikisha vinakamilisha marejesho, akisisitiza kuwa hatua hiyo italenga kuwezesha wananchi wengine kunufaika na mfuko huo.

Akizungumza Julai 1, 2026 katika Baraza Maalum la Madiwani la kujadili hoja za Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Mrindoko amesema hoja ya mikopo isiyorejeshwa yenye thamani ya takribani Sh bilioni 1.14 haiwezi kuendelea kuvumiliwa.
Amesema Serikali inafahamu vikundi vyote vilivyokopeshwa, hivyo hakuna sababu ya wanufaika kushindwa kutimiza wajibu wao wa kurejesha fedha zilizotolewa kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi.
“Fedha hizi ni za mzunguko. Zikirejeshwa zitawanufaisha wananchi wengine wenye sifa za kupata mikopo. Hivyo kila kikundi kinachodaiwa kinapaswa kurejesha fedha hizo ndani ya siku 90,” amesema.
Mrindoko ameagiza wanufaika wote waliokimbia au kuficha makazi yao watafutwe kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, huku akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kuwasilisha ndani ya siku 14 orodha ya vikundi na watu binafsi wanaodaiwa ili hatua za kisheria na kiutawala zichukuliwe.
Mbali na hilo, amesisitiza watumishi wa umma kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao, akielekeza kuwa watumishi watakaobainika kusababisha hoja za ukaguzi wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Aidha, ameitaka halmashauri kuhakikisha miradi yote iliyopokea fedha za Serikali inakamilika ndani ya miezi mitatu na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Albert Msovela, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa kufikia asilimia 100 ya malengo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupata hati safi ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2024/25, akisema mafanikio hayo yanapaswa kuambatana na uwajibikaji zaidi katika usimamizi wa fedha za umma.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, amesema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itaendelea kushirikiana na Baraza la Madiwani na Menejimenti ya Halmashauri ili kuimarisha utendaji na kudumisha nidhamu ya matumizi ya rasilimali za Serikali.


