27 C
New York

Yanga, Simba zasubiriana kwenye kona ubingwa NBC

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

SASA ni wazi Yanga na Simba zitasubiri hadi keshokutwa Juni 30, 2026, ili kujua utakakoelekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2025-26.

Ni baada ya matokeo ya mechi za jana Juni 27, 2026, Yanga ikiwa nyumbani katika Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya TRA United.

Simba nao walikusanya pointi tatu walipoifunga Singida Black Stars mabao 2-0 kule Meja Jenerali Isamhuyo.

Kwa hesabu zilivyo, baada ya kila timu kucheza mechi 29 na kubakiza moja, mabingwa watetezi, Yanga, wako kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 72.

Simba, kwa upande wao, wako nafasi ya pili kwenye msimamo huo wa Ligi kwa tofauti ya pointi mbili pekee.

Hivyo basi, kwa mujibu wa ratiba, timu zote zitashuka dimbani keshokutwa kumaliza msimu huu wa Ligi, ambapo Yanga watarudi Jenerali Isamhuyo kuvaana na JKT Tanzania.

Siku hiyo hiyo, Wekundu wa Msimbazi wao watakuwa na kibarua dhidi ya ‘Wakusanya Mapato’ wa Kinondoni, KMC.

HESABU ZA UBINGWA

Endapo Yanga itaifunga JKT, basi itafikisha pointi 75 na kutwaa ubingwa kwa kuwa Simba haitoweza kuzifikia hata kama itapata ushindi mbele ya KMC.

Pia, ikitokea Yanga kufungwa,l kisha Simba ikashinda, basi itafikisha pointi 73, hivyo ubingwa wa msimu huu utaelekea Msimbazi.

Ikitokea sare kwa timu zote, kwa maana ya Yanga (dhidi ya JKT) na Simba (dhidi ya KMC), basi ‘ndoo’ itatua Yanga kwa tofauti iliyopo sasa ya pointi mbili.

Lakini, ikitokea Yanga ikalazimishwa sare, kisha Simba ikashinda, vigogo wa Kariakoo watalingana pointi (73), hivyo hesabu za wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa zitachukua nafasi yake.

Kwa sasa, ‘Timu ya Wananchi’ ina wastani mzuri wa mabao 59 dhidi ya 42 waliyonayo wenzake wa Simba.

YANGA V JKT

JKT Tanzania wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi, wakiwa na pointi 42 katika mechi zao 29.

Hata hivyo, rekodi yao mbele ya Yanga haiwapi matumaini makubwa ya kupata sare, achilia mbali ushindi, katika mchezo wa keshokutwa.

Katika mechi 10 za hivi karibuni dhidi ya Yanga, JKT haijaweza kuambulia ushindi, na badala yake imefungwa saba na kutoa sare tatu.

Mechi ya hivi karibuni ni ile ya Mei 16, 2026, ambapo Yanga walishinda mabao 2-0 katika michuano ya Kombe la FA.

Kwenye Ligi msimu huu, timu hizo zilikutana Februari 25, 2026, na Yanga kuzoa pointi tatu kwa ushindi mnono wa mabao 5-0.

SIMBA V KMC

Haionekani mechi ngumu kwa Simba. KMC imeshashuka daraja na iko mkiani mwa msimamo wa Ligi ikiwa imekusanya pointi tisa pekee baada ya mechi zake 29.

Simba watashuka dimbani wakiwa na mfululizo wa kushinda mechi tano mfululizo. KMC haijaonja ushindi zaidi ya vipigo katika michezo yote mitano iliyocheza hivi karibuni.

Hata rekodi za KMC mbele ya Simba zinathibitisha mechi ya keshokutwa ilivyo ya upande mmoja.

Katika mechi 10 walizokutana na Wekundu wa Msimbazi, KMC wamefungwa nane na kuambulia sare mbili pekee.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana, ilikuwa Februari 11, 2026, ambapo ulikuwa mchezo wa raundi ya kwanza msimu huu wa Ligi na Simba kushinda mabao 2-0.

Related articles

Recent articles