Na Hassan Mwasha, Gazetini
UKIKATIZA mitaa miwili hadi mitatu, hasa katika majiji makubwa kama ilivyo kwa hapa Dar es Salaam, ni jambo lisilowezekana kukutana na moja ya makundi hayo.
Kama si kukutana na watoto wa mitaani, basi utakutana na warahibu wa dawa za kulevya ‘mateja’, au chaka la mabinti/wanawwke ‘waliojiajiri’ kupitia huduma ya ngono.
Kwa lugha nyingine na rahisi kueleweka, makundi hayo ni moja ya alama zinazoweza kutumika kutambulisha majiji makubwa hapa nchini.
Kwa nyakati tofauti, mamlaka zimeonesha dhamira (sioni kama ni ya dhati) katika kukabiliana na utitiri wa watu wa aina hiyo katika jamii.

Wakati fulani, Jiji la Dar es Salaam lilikuwa na operesheni nzuri mno na ya kupigiwa mfano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya.
Kwa kiasi kikubwa, ‘mateja’ walipungua mitaani na kuonekana wangeisha kabisa endapo operesheni ile iliyosimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa wakati huo, Paul Makonda, ingekuwa endelevu.
Baadaye, iliota mbawa na maisha yakaendelea. Utaratibu wa kupishana na mateja kila kona ukarudi kwa kasi na unaendelea hadi sasa.
Kwa upande wa watoto wa mitaani, kampeni za kutokomeza janga hilo zimekuwa za kisiasa, badala ya dhamira ya dhati.
Ni kauli ambazo zimekuwa zikiishia Bungeni na kutumika kama karata ya ushindi wa hoja, huku idadi ya watoto wasio na makazi maalumu ikibaki pale pale au kuongezeka zaidi.
Leo hii, kila kona ya barabara kubwa kumejaa watoto wa mitaani, tena wengi wao wakiwa na umri wa kuhitaji malezi ya wazazi au kuwa shuleni. Hakuna anayejali.
Ahadi za viongozi na mamlaka juu ya kutokomeza tatizo hilo zimebaki kwenye makarabrasha, licha ya hatari kubwa kwa jamii kuendelea kuishi na vijana hao.
Vijana wasio na elimu, wasioiona kesho yao, waliokata tamaa, na kujichukulia kama kundi lililotengwa na mfumo halisi na sahihi wa maisha katika jamii.
Mamlaka zinafahamu matokeo yake? Kama jibu ni nsiyo, kwanini bado zinaendelea ‘kuichukulia poa’ changamoto hiyo?
Ni kama ilivyo pia kwa ‘madada poa’. Walau miaka mingi iliyopita, walitega biashara yao katika maeneo maalumu, mbali na makazi ya watu.
Vipi sasa? Hali ni mbaya. Katikati ya makazi ya watu, biashara ya ukahaba imekuwa ikifanyika pasi na kificho, kiasi kwama hata watoto wanaona kinachoendelea. Hii ni hatari.
Tujiulize; mamlaka ziko wapi? Zimeishia wapi zile operesheni za kuvamia na kuharibu ‘vijiwe’ vya makahaba? Na je, ni nani anayesubiriwa kusema ili ziwe za kudumu?


