PRETORIA, Afrika Kusini
AFRIKA Kusini ina wahamiaji zaidi ya milioni tatu, sawa na asilimia 5 ya watu wote nchini humo, wengi wakitokea nchi za Kusini, ziikiwamo Zimbabwe, Zambia na Malawi.
Kwa wiki kadhaa sasa raia wa kigeni walioingia na kuishi Afrika Kusini kwa ‘njia za panya’ wamekuwa wakipitia nyakati ngumu, ikiwamo kuporwa mali, kujeruhiwa na hata kuuawa.
Matendo hayo yanafanywa na wazawa, hasa vijana, wanaoshinikiza raia wa kigeni kuondoka katika nchi yao kwa madai mbalimbali.
Mosi, wanasukumwa na madai ya wageni kupora ajira zao. Afrika Kusini ni moja ya mataifa yenye kiwango kikubwa (32.7%) cha uhaba wa ajira kwa vijana.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa nchi hiyo imepoteza ajira 350,000 katika Robo ya Kwanza ya Mwaka 2026
Pili, wanaamini uwepo wa wageni umeathiri upatikanaji wa huduma bora za kijamii (afya, maji, umeme, n.k.)
“Tunashindwa kumudu gharama za kupeleka watoto shule. Tunashindwa hata kumudu kuwapeleka wazee wetu hospitali,” anasema mmoja ya waandamanaji, Mecha Ramorola.
HALI HALISI
Esnat Joseph (36), raia wa Malawi, anaeleza kuwa kwa sasa anaishi kwa hofu. “Naogopa na nimeteswa kisaikolojia,” anasema.
“Watu (nisowafahamu) walinivamia nyumbani na kuniambia ‘unatakiwa kuondoka. Hatutaki mkae hapa tena, nendeni kwenye nchi yenu’,” anasimulia Esnat.
Kwa mujibu wa mwanamke huyo anayeishi Durban, watu hao walikuwa 10 na walishika silaha walizotumia kumjeruhi mume wake kichwani na shingoni.
“Walimshika shingo kama vile wanataka kumuua. Kwa sababu ya Mungu, bado anaishi, ingawa yuko hospitali,” anasisitiza.
Kutokana na hofu, baadhi ya wageni wamelazimika kuweka makazi nje ya Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani mjini Durban.
Mwanamke raia wa Burundi, ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, amesema: “Nahofia kupoteza maisha. Watoto wangu wanahofia pia.”
Aidha, mwanamke mwingine raia wa Malawi, ambaye amekuwa akiishi na kufanya kazi mjini Cape Town kwa miaka 16, anasema mtoto wake haendi tena shule akihofia kushambuliwa au hata kuuawa.
Benjamin, ambaye amerejea Lagos, Nigeria, baada ya miaka tisa ya kuishi Afrika Kusini, anasema:
“Waafrika Kusini hawapendi raia wa kigeni, hasa Wanigeria. Afrika Kusini siyo sehemu ya kuishi, ni sehemu unayoweza kupoteza maisha wakati wowote.”
UTETEZI WAO
Waratibu wa maandamano wanajitetea wakisema hawachukii wageni kuingia Afrika Kusini, bali wanataka sheria za nchi yao ziheshimiwe.
Jacinta Ngobese-Zuma, ambaye ni mmoja ya viongozi, anasema: “Kama ulikuja na hati ya kusafiria inayotaka ukae siku 30, halafu zikawa 50, miaka miwili hadi mitano, unakuwa umevunja sheria.
“Sasa, hatuwezi kuwa na Afrika Kusini iliyogeuzwa kituo cha wakimbizi wa nchi zingine zilizofeli. Kila nchi inajali wananchi wake, tunataka iwe hivyo pia kwa Afrika Kusini,” amesema.
Hata hivyo, zipo ripoti za hata wageni wenye nyaraka halali nao kushambuliwa katika maeneo kadhaa.
“Nina nyaraka zote za kuishi kama mkimbizi hapa Afrika Kusini, lakini sote tunakimbizwa,” anasema mwanamke raia wa Burundi akiwa na watoto wake wanne.
NGUVU YA SIASA
Aidha, nyuma ya vijana hao, siasa zimehusika kwa kiasi kikubwa. Kabla ya matukio hayo, baadhi ya vyama vya upinzani, kikiwamo ActionSA.
Chama hicho kinashikiza raia wa kigeni wanaoishi Afrika Kusini kinyume cha sheria kurejea makwao kabla ya Juni 30, 2026.
Miaka mitano iliyopita, kiongozi wa ActionSA, Herman Mashaba, alieleza kuwa raia wa kigeni milioni 15 wanaishi Afrika Kusini bila kufuata utaratibu.
Wakati huo, waandamanaji wakiwa na bakora mikononi waliimba ‘Mabahambe’, neno la Kizulu lenye maana ya ‘Wanatakiwa Kuondoka’.
Kwa upande mwingine, mwanasheria wa haki za binadamu nchini Afrika Kusini, Sharon Ekambaram, anazungumzia namna wanasiasa wanavyochangia vurugu dhidi ya wageni, akisema:
“Vyama vya siasa vinajaribu kudanganya watu kwamba matatizo yetu yote yanatokana na wahamiaji, kwamba wakiondoka hatutakuwa na shida yoyote.”
HATUA ZILIZOCHUKULIWA, KAULI YA RAIS
Wiki za hivi karibuni zimeshuhudia mataifa ya Ghana, Msumbiji, Nigeria na Zimbabwe yakisafirisha raia wake na kuwarejesha nyumbani.
Safari za ndege na basi zimefanikisha raia wa kigeni takribani 3,500 kuondoka katika ardhi ya Afrika Kusini.
Mapema wiki hii, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, aliwaasa vijana, akiwaaambia raia wa kigeni si chanzo cha matatizo yao.
“Afrika Kusini haina nafasi kwa vitendo vya chuki dhidi ya wageni, ubaguzi wa rangi na jinsia au aina nyingine yoyote ya ubaguzi,” alisema.
HISTORIA INAYOJIRUDIA
Hii si mara ya kwanza kwa raia wa kigeni kupitia aina hiyo ya mateso nchini Afrika Kusini. Machafuko ya mwaka 2008 yalisababisha vifo 62.
Pia, matukio ya aina hiyo yalijitokeza tena katika miaka ya 2015, 2016 na 2019, yalisababisha maelfu ya wageni kukimbilia makwao.


