16.9 C
New York

Nani anayezalisha ‘wanyonge’ wanaomsumbua Waziri Mkuu?

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

NIMEKUWA nikifuatilia kwa karibu ziara za Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, tangu alipoanza kuzunguka katika mikoa mbalimbali nchini.

Tutakubaliana kuwa huo siyo utamaduni mpya, hivyo sioni hoja ya wanamuona Waziri Mkuu kama mtu wa ajabu katika hicho anachokifanya – ziara za kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Ni mapema mno kusahau kuwa hiyo ilikuwa silaha kubwa ya Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Pombe Magufuli, ambaye aliitumia vizuri kuvuna ushawishi mbele ya ‘wanyonge’ wa nchi hii.

Hivyo basi, itoshe kusema Waziri Mkuu hajaja na jambo la tofauti, kiasi cha wakosoaji kumshangaa na kumuona ni mtu wa ajabu. Ni njia ile ile ya Hayati Dk. Magufuli na viongozi wengine wa Serikali na hata CCM wakati mwingine.

Na badala yake, mjadala unaoweza kuwa na tija ni namna ‘wanyonge’ walivyobaki pale pale, wakisubiri ziara za wakubwa ili kutetewa, kupozwa na kupewa tumaini jipya katika madhila yanayowakabili.

Kwamba bado wananchi wanaishi kwenye unyonge mkubwa mbele ya watendaji wa Serikali wa ngazi za chini, kiasi cha kuweka imani yao yote kwa Waziri Mkuu au kiongozi mwingine wa juu, akiwamo Makamu wa Rais au Rais mwenyewe.

Iko hivi; ukifuatilia ziara ya Waziri Mkuu, asilimia kubwa, kama si zaidi ya 70, ya kero za ‘wanyonge’ zinachomoza zikiwa na sura moja inayogusa maeneo mawili tu.

Mosi, kero hizo zina uhusiano wa moja kwa moja na uwajibikaji hafifu wa viongozi au mamlaka za eneo husika. Waziri Mkuu anapokutana na kero ndogo ya mgogoro wa kiwanja iliyodumu miaka miwili au zaidi, jibu rahisi ni kutokuwajibika kwa mamlaka za chini na si vinginevyo.

Bila kupepesa macho, viongozi wa eneo hilo, kuanzia Kata, Wilaya hadi Mkoa, ndiyo waliosababisha unyonge kwa kushindwa kumaliza changamoto hiyo.

Kuthibitisha hilo, katika baadhi ya kero kwa Waziri Mkuu, ‘wanyonge’ wameeleza pia walivyofika kwa wakuu wa wilaya na mikoa lakini bado zilikosa ufumbuzi kutokana na uwajibikaji hafifu.

Mathalan, wapo waliokiri kufunga safari kutoka mkoa wanayoishi hadi mwingine ili kuuwahi mkutano wa Waziri Mkuu, wakiamini watapata nafasi ya kusikilizwa.

Inashanga kusikia kwamba kero zingine zilihusu mgogoro wa wanafamilia wanaogombea nyumba au mali zingine za urithi. Hilo nalo ni suala linalohitaji uwepo wa Waziri Mkuu? Viongozi au mamlaka za eneo hilo zina kazi gani?

Pili, ni kero zenye sura ya ubabe na ukiritimba kwa baadhi ya watumishi wa umma. Akiwa mkoani Singida, moja ya kero zilizoibuliwa na ‘wanyonge’ ni mamlaka fulani ya udhibiti kuchukua na kushikilia madumu ya mafuta ya wafanyabiashara.

Si tu ilikiuka agizo la awali la Waziri Mkuu, kwamba wafanyabiashara wasipokonywe bidhaa zao, bali pia mamlaka hiyo ilitoa picha nyingine isiyofaa, licha ya kuwapo kwa miaka mingi katika uhusiano wa ‘wanyonge’ na watumishi wa umma.

Mamlaka hiyo ilithibitisha namna baadhi ya watumishi wa umma walivyoachana na utamaduni wa mazingira rafiki ya kuhudumia, na badala yake kuvaa ‘sura ya jeshi’ mbele ya ‘wanyonge’.

Hivyo, kitendo cha kusubiri ziara za wakubwa, kama ilivyo kwa Waziri Mkuu, kinatoa picha ya namna ‘wanyonge’ walivyopoteza imani na watendaji wa Serikali wa ngazi za chini, ambao kimsingi ndiyo walio nao karibu zaidi, ikilinganishwa na Waziri Mkuu.

Katika mazingira ya aina hiyo, Serikali yoyote duniani haipaswi kujivunia. Kwa namna moja au nyingine, ni mazingira yanayoashiria anguko la ‘system’ (mfumo) wa kiutendaji katika sekta ya utumishi wa umma.

 

Related articles

Recent articles