16.9 C
New York

Thomas Tuchel: Kutoka uhudumu wa baa hadi ukocha Kombe la Dunia

Published:

LONDON, Uingereza

WAKATI timu ya soka ya Taifa ya England inacheza Kombe la Dunia mwaka 1998, kocha wao wa sasa, Thomas Tuchel, alikuwa muhudumu wa baa moja mjini Stuttgart, Ujerumani.

Kocha mwenye heshima kubwa nchini humo, Ralf Rangnick, ambaye wakati fulani alipita Manchester United, anaikumbuka vizuri stori hiyo.

Tuchel akiwa beki wa SSV Ulm iliyokuwa timu ya madaaka ya chini Ujerumani katika miaka ya 1990, alicheza chini ya kocha huyo.

Hata hivyo, majeraha na operesheni ya goti akiwa na umri wa miaka 23 vilimfanya aachane na soka akiwa na maumivu ya kutokutimiza ndoto yake ya kucheza Bundesliga.

“Nilipostaafu, sikuwa na chochote kwenye akaunti ya benki. Sikuwa na njia nyingine zaidi ya kutafuta kazi ya kuendesha maisha,” alisema Tuchel.

Katika kutafuta ajira yoyote ile ili kumudu gharama za maisha, ndipo alipojikuta kwenye uhudumu wa baa. Akiwa hapo, anakumbuka ilivyomuuma kuona SSV inapanda daraja na kuingia Bundesliga mwaka 1999.

“Iliniuma sana kwa sababu nilihisi nilipaswa kucheza Bundesliga, niliona wanaiishi ndoto yangu. (Siku hiyo) Nikifanya kazi kwa nusu tu baada ya kusikia taarifa hiyo, nikaaga na kurudi zangu nyumbani,” alisema.

Siku moja Tuchel akiendelea na majukumu yake kwenye baa hiyo iliyokuwa maarufu na kutembelewa na mastaa, mmoja ya wateja alikuwa Rangnick.

Rangnick anasimulia akisema: “Nilishangaa kumkukuta pale akifanya uhudumu ili kupata pesa ya kula. Nilimuomba aachane na kazi hiyo na kurejea kwenye soka.”

Huo ulikuwa ni mwanzo wa safari mpya ya maisha ya Tuchel kwani Rangnick alimkutanisha na mkurugenzi wa ‘academy’ ya klabu ya VfB Stuttgart aliyokuwa akiinoa wakati huo.

“Nilimkutanisha na mkurugenzi wa ‘academy’ na huo ukawa mwanzo wa safari yake ya ukocha,” anasema Rangnick.

Tuchel alikabidhiwa vijana wa U-15, kabla ya kupandishwa na kuwa msaidizi wa kocha wa U-19 wakati huo, Hans-Martin Kleitsch.

Ni wakati huo, waliweza kuibua vipaji vingi, wakiwamo Sami Khedira na Mario Gomez, wakati U-19 yao ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani ya vijana mwaka 2005.

Kuanzia hapo, maisha yalibadilika na sasa Tuchel ni miongoni mwenye ‘CV’ ya kufanya kazi na klabu kubwa za Ulaya za Borussia Dortmund, Chelsea, PSG na safari hii analiongoza benchi la ufundi la ‘Three Lions’ katika fainali za Kombe la Dunia.

Related articles

Recent articles