Na mwandishi wetu, Gazetini
KUFIKIA hatua hii ya msimu wa 2025-26 wa Ligi Kuu Bara, zimeshachezwa jumla ya mechi 400, kila timu ikishuka dimbani mara 25 na kubakiza mechi tano.
Katika mechi hizo, vimeshuhudiwa vipigo 139, sawa na asilimia 34.75 ya mechi zilizochezwa katika viwanja mbalimbali vya Dar es Salaam na mikoani.
Takwimu ziko hivi; katika vipigo hivyo 139, KMC ikiongoza kwa kufungwa mara 20, sawa na asilimia 80 ya mechi zake 25.
Katika nafasi ya pili, ni vigogo wa soka la Mbeya, Tanzania Prison, ambao wamechezea vichapo 15, sawa na asilimia 65, na Mbeya City iliyopoteza mara 13 (52%).
Timu zingine zilizofungwa mechi nyingi msimu huu ni Fountain Gate iliyopoteza mara 12, sawa na asilimia 48 ya mechi 25 ilizocheza kufikia hatua hii ya msimu.
Coastal Union inafuata ikiwa imefungwa mechi 11 kati ya 25 (44%), na Mtibwa Sugar na Namungo, ambazo kila moja imetandikwa mara 10 (40%).
Kwa upande mwingine, Yanga na Simba, pamoja na matajiri wa Chamazi, Azam, ndiyo timu tatu pekee zilizofungwa mara moja kila moja, sawa na asilimia 4 ya mechi zao.
Yanga, mabingwa watetezi, bado wamejichimbia kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 60, wakiizidi mbili Simba inayoshika nafasi ya pili.


