WASHINGTON DC, Marekani
JUNI 7, 2026) zilitimia siku 100 tangu Marekani kwa kushirikiana na Israel zilipoanzisha mashambulizi dhidi ya Iran, vita vilivyosababisa kupanda kwa bei ya mafuta na kutikisa kwa kiasi kikubwa uchumi wa dunia.
Kuongeza hali tete Mashariki ya Kati, pia Israel iko kwenye mapigano makali na Lebanon, ambako inashambuliana na kundi la kigaidi nchini humo, Hezbollah.
Ikumbukwe, Hezbollah waliingia vitani kuwasaidia washirika wake, Iran, baada ya kuvamiwa na Marekani na Israel.
Tangu Aprili 8, 2026, yamekuwapo makubaliano kadhaa ya kusitisha vita, lakini pande mbili hizo zimeshuhudiwa zikiendelea kushambuliana kwa nyakati tofauti.
Taarifa rasmi kutoka mamlaka za Lebanon zinaeleza kuwa mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 3,000.
ULAYA YAJIWEKA KANDO
Kwa kipindi chote cha siku 100 za vita, washirika wa Marekani barani Ulaya hawajaonekana kushiriki vita hivyo dhidi ya Iran.
Na badala yake, mataifa mengi yamehimiza kupatikana kwa suluhu ya kidiplomasia ili kuondosha changamoto iliyopo ya uhaba na kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta duniani.
Wakati huo huo, Urusi na China, washindani wakubwa wa Marekani katika nyanja ya kiuchumi, nao hawajaingia vitani, licha ya kila moja kutoa maoni yake ya kutaka hali ya amani irejee huko Mashariki ya Kati.
HALI TETE MASHARIKI YA KATI
Licha ya vita kuzihusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran na Lebanon, mataifa mengine ya Mashariki ya Kati yameingia kwenye changamoto kubwa ya hali mbaya ya usalama.
Iran imekuwa ikizishambulia nchi zenye ushirikiano na Marekani, zikiwamo Oman, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Kuwait, Jordan, na Saudi Arabia.
Mathalan, Oman walishuhudia bandari zao mbili, Duqm na Salalah, zikishambuliwa na ndege zisizo na rubani, kisha shambulizi lililoua raia wawili wa kigeni katika Jimbo la Sohar katika tukio la Machi 13, 2026.
Iran, ambao ni marafiki wakubwa na Oman, walikana kuhusika katika mashambulizi hayo, huku swali la nani aliyehusika kati yao, Marekani na Israel likikosa majibu.
Qatar nayo ilishambuliwa katika kinu chake cha gesi asilia (LNG), ikiituhumu Iran kuhusika. Kutokana na shambulizi hilo, Qatar iliwatimua viongozi wa kijeshi na kidiplomasia wa Iran nchini humo.
Marekani na Israel nazo zimekuwa zikielekeza mashambulizi ya makombora kwa nchi zenye uhusiano wa karibu na Iran.
Mathalan, Iraq ambayo imekuwa karibu na Iran tangu kuondoshewa madarakani kwa Rais Saddam Hussein mwaka 2003, imeshuhudia wapiganaji wake, PMF, wakishambuliana na Marekani.
MTAZAMO WA AFRIKA
Licha ya kutokushiriki vita, mataifa ya Afrika yametikiswa kwa kiasi kikubwa na kile kinachoendelea huko Mashariki ya Kati. Afrika inaagiza asilimia zaidi ya 70 ya mafuta yaliyo tayari kwa matumizi.
Aprili, 2026, ripoti ya moja ya tafiti ilitahadharisha kuwa huenda Afrika ikawa na uhaba wa tani milioni 86 za mafuta kufikia mwaka 2040.
Misri imeeleza matamanio yake ya kuona mgogoro wa Mashariki ya Kati ukipatiwa ufumbuzi kutokana na athari zake kwenye uchumi wa dunia.
Hiv karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Taifa hilo la Afrika ya Kaskazini, Badr Abdelatty, alifanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Iran.
Machi, 2026, Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi, alizungumza na Donald Trump na kumwambia: “Wewe tu ndiye unayeweza kumaliza mgogoro huu.”
Umoja wa Afrika (AU) nao umezitaka pande zote zinazohusiana na mgogoro wa Mashariki ya Kati kumaliza tofauti zao kwa njia ya kidiplomasia.


