23.5 C
New York

Kijiji cha Rung’abure chatekeleza miradi ya zaidi ya Sh bilioni 1.2

Published:

Na Malima Lubasha, Serengeti

KIJIJI cha Rung’abure kilichopo Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, kimetekeleza na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.247 katika sekta za afya, elimu na maji kuanzia mwaka 2016 hadi 2025.

Miradi hiyo imelenga kuboresha huduma za kijamii kwa wakazi wa kijiji hicho na kupunguza changamoto zilizokuwa zinawakabili wananchi katika upatikanaji wa huduma muhimu.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Marwa Meng’anyi, alisema hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.

Alisema fedha zilizotumika katika miradi hiyo zimetokana na Serikali Kuu, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, michango ya wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Meng’anyi aliipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za maendeleo vijijini na kuahidi kuwa viongozi wa kijiji wataendelea kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kuwa ni ujenzi wa zahanati, shule shikizi ya Nyamemba pamoja na uboreshaji wa miundombinu katika Shule ya Msingi Geitasamo.

Alisema uamuzi wa kujenga zahanati ulitokana na wananchi, hususan wanawake wajawazito, kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika vijiji vya jirani.

Aidha, alisema hadi sasa vyumba 14 vya kutolea huduma za afya vimekamilika katika zahanati hiyo.

Kwa upande wa elimu, alisema ujenzi wa Shule Shikizi ya Nyamemba umetokana na malalamiko ya wazazi kutoka vitongoji vya Nyamemba na Keregero waliokuwa wakilazimika kuwapeleka watoto wao umbali wa zaidi ya kilometa 10 kwenda Shule ya Msingi Geitasamo.

“Mpaka sasa zaidi ya shilingi milioni 70 zimetumika katika ujenzi wa zahanati, zaidi ya milioni 100 katika shule shikizi ya Nyamemba na zaidi ya milioni 70 katika uboreshaji wa miundombinu ya Shule ya Msingi Geitasamo,” alisema Meng’anyi.

Aliongeza kuwa kati ya vitongoji vinane vya kijiji hicho, vitano tayari vimepata huduma ya umeme huku mipango ya kupeleka umeme katika vitongoji vilivyosalia ikiendelea.

Pia alisema kijiji kinaendelea na maandalizi ya kuanza ujenzi wa shule mpya ya sekondari baada ya kupitishwa na mkutano mkuu wa kijiji.

Kuhusu huduma ya maji, Meng’anyi alisema Benki ya Dunia ilitoa Shilingi milioni 950 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji ya mtiririko katika eneo la Nyamemba kupitia RUWASA Wilaya ya Serengeti.

Alisema mradi huo umehusisha ujenzi wa tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 pamoja na usambazaji wa mabomba katika vitongoji vyote vya kijiji.

Kwa sasa zaidi ya wakazi 4,000 kutoka kaya 817 wanapata huduma ya maji safi na salama.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliliambia gazeti hili kuwa miradi inayotekelezwa imekuwa na manufaa makubwa kwa jamii, huku wakieleza kuwa wananchi hushirikishwa katika vikao vya kijiji kujadili na kutoa maamuzi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Pia walieleza kuwa hali ya ulinzi na usalama kijijini humo ni nzuri kutokana na uwepo wa amani na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Related articles

Recent articles