Na Hassan Mwasha, Gazetini
WAKATI Uganda na Kenya zikiwa zimeshapata mabingwa wa msimu huu katika Ligi Kuu zao, hapa nchini bado ‘ugali moto, mboga moto’ katika vita ya vigogo wa Kariakoo, Yanga na Simba.
Ushindi wa mabao 31 dhidi ya Namungo katika mchezo wa jana Mei 25, 2026 umeirudisha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Simba inayoshika nafasi pili.
UGALI MOTO, MBOGA MOTO
Kwa mujibu wa msimamo, Yanga wamefikisha pointi 60, Simba wana 58, huku kila timu ikiwa imeshashuka dimbani mara 25 na kubakiza mechi tano tu kumaliza msimu huu wa 2025-26.
Katika mechi 25, Yanga imeshinda 18, sare sita na kufungwa moja, ikifunga mabao 59 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.
Kwa upande wa Wekundu wa Msimbazi, Simba, katika mechi 25 walizoshuka dimbani, wamepata ushindi mara 17, sare saba na kufungwa moja. Mabao ya kufunga ni 44 na ya kufungwa ni 10.
Baada ya kumalizana na Namungo, kituo kinachofuata kwa Yanga kwenye mechi za Ligi Kuu ni Kigoma, ambako wataifuata Mashujaa.
Siku moja baada ya mechi hiyo ya Juni 13, 2026, Simba nao watashuka dimbani, safari hii wakiialika Pamba Jiji katika nyasi za Uwanja wa KMC, Mwenge jijini Dar es Salaam.
LIGI KUU YA UGANDA
Msimu wa 2025-26 wa Ligi Kuu ya soka nchini Uganda ulitamatika Mei 23, 2026 kwa Vipers SC kutwaa ubingwa baada ya kuifunga Express mabao 2-0.
Hata hivyo, Vipers walishatangazwa kuwa mabingwa tangu Mei 20, 2026 walipopata ushindi wa mabao 3-0 katika mechi yao ya 29 dhidi ya Maroons, ambapo walifikisha pointi 64.
Kwa kuifunga Express, Vipers, mabingwa mara nane wa Ligi Kuu ya Uganda, walifikisha pointi 67, wakiizidi tano KCCA iliyomaliza msimu ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo.
Katika mechi 30 za Ligi walizocheza, walishinda 19, sare 10 na kufungwa moja, wakifunga mabao 55 na kuruhusu 17. Kwa upande wao, KCCA walishinda 19, sare tano, vipigo sita, wakifunga mabao 46 na kuruhusu 22.
LIGI KUU YA KENYA
Huku kila timu ikiwa imebakiza mechi moja kufunga msimu ifikapo Mei 31, 2026, tayari Gor Mahia wameshajihakikishia ubingwa baada ya kufikisha pointi 68. FC Leopards wako nafasi ya pili wakiwa na pointi 64.
Gor Mahia, walioshiriki msimu huu wakiwa mabingwa watetezi, walitangaza ubingwa Mei 24, 2926 baada ya wapinzani wao hao, FC Leopards, kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa APS Bomet.
Hivyo, wakongwe Gor Mahia wanafikisha ubingwa wao wa 22, ikiwa ndiyo timu yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya Kenya.
Katika mechi zao 32 katika Ligi hiyo ya timu 18, Gor Mahia imeshinda 20, imetoa sare nane na kufungwa nne. Mabao ya kufunga ni 50 na ya kufungwa ni 21.


