17.1 C
New York

Mambo 5 yaliyoipa Arsenal ubingwa wa EPL

Published:

LONDON, Uingereza

MATESO yamekwisha. Baada ya miaka 22 ya kusubiri, Arsenal imetwaa taji la Ligi Kuu ya England (EPL). Taji hilo limetua Emirates baada ya washindani wao wakubwa msimu huu, Manchester City, kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Bournemouth.

Kwa sare hiyo, Arsenal sasa wamefikisha pointi 82, ambazo Man City yenye 78 haiwezi kuzifikia hata kama itashinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Aston Villa.

Makala haya yanaangazia mambo 5 yaliyowawezesha Washika Bunduki hao wa London kubeba taji la EPL kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004.

Ubingwa ambao umekuja wakiwa wameshinda mechi 25 kati ya 37, wakitoa sare saba na kufungwa tano pekee, mafanikio yaliyotokana na uwekezaji wa Pauni milioni 250 katika soko la usajili kuwanasa Viktor Gyokeres, Martin Zubimendi, Piero Hincapie, Noni Madueke na Eberechi Eze.

MWENDO WA KUFUNGA MABAO, ‘UKUTA’ IMARA

Arsenal wametwaa ubingwa lakini moja ya maeneo waliyokuwa bora msimu huu ni idara ya mabao, ambapo wamezifumania nyavu mara 69 katika mechi 37 za EPL.

Kama hiyo haitoshi, safu yao ya ulinzi imeweka rekodi ya kuruhusu mabao machache zaidi ndani ya msimu mmoja wa Ligi Kuu hiyo. Mabao 26.

RAYA, SALIBA KIBOKO

Mlinda mlango David Raya ameokoa nafasi za wazi 60 (69%), pia akicheza mechi 19 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa. Ameshachukua tuzo tatu za Kipa Bora, akisubiri moja kuwafikia wakongwe Petr Cech na Joe Hart.

Beki wa kati, William Saliba, naye alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Arsenal msimu huu. Katika mechi 31 alizokuwa uwanjani, timu hiyo iliruhusu mabao 20 pekee, huku 15 zikimalizika bila kuruhusu bao.

RICE APEWE MAUA YAKE

Katika mechi alizocheza Declan Rice, Arsenal ilikuwa na utulivu mkubwa kwenye eneo la kiungo, hasa kwa uwezo wake wa ‘kukata umeme’ na kurudisha mipira iliyopotea.

Kama hiyo haitoshi, Rice amefunga mabao sita na kutoa ‘asisti’ nane kuwasaidia Washika Bunduki katika mapambano ya kuwania taji la EPL msimu huu wa 2025-26.

MIPIRA YA KUTENGA

Arsenal imefunga mabao 17 yanayotokana na kona msimu huu na kuvunja rekodi yao ya mabao 16 waliyopachika misimu miwili iliyopita (2023-24). Kwa ujumla, zikiwamo na faulo, imefunga mabao 28 katika mechi 37.

Katika shughuli hiyo, Rice ndiye silaha yao kubwa, ambapo amefunga mabao matano na kutoa asisti nne kwa staili hiyo ya mipira iliyokufa.

NIDHAMU NDANI YA UWANJA

Mafanikio ni matokeo ya nidhamu katika kile unachokifanya. Kwa msimu mingi waliyokaribia kutwaa ubingwa wa EPL hivi karibuni, Washika Bunduki waliponzwa na matukio mengi ya utovu wa nidhamu ndani ya uwanja.

Safari hii, mambo yamekuwa tofauti. Arsenal wanaelekea kumaliza msimu wakiwa hawana kadi nyekundu katika michezo yote 37 waliyoshuka dimbani msimu huu wa EPL.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img