10.5 C
New York

DCEA yateketeza ekari 68 za bangi Tabora

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tabora, imefanya operesheni maalum katika hifadhi ya msitu wa Igombe River iliyopo Wilaya ya Uyui na hifadhi ya msitu wa Nyahua iliyopo Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, na kufanikiwa kuteketeza ekari 68 za mashamba ya bangi, kukamata gunia 133 za bangi pamoja na kuwakamata watu saba wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo haramu.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 30, 2026 katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mamlaka hiyo kwa sasa ipo kwenye operesheni maalum ya kuteketeza dawa za kulevya zinazozalishwa ndani ya nchi kama sehemu ya mapambano mapya baada ya kudhibiti kwa kiasi kikubwa dawa za kulevya za viwandani zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.

“Sasa hivi tuko kwenye kampeni maalum kuhakikisha kwamba tunateketeza dawa za kulevya zinazozalishwa nchini baada ya dawa za viwandani kupungua,” amesema Lyimo.

Aidha, Lyimo amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha DCEA kuanzisha ofisi ya Kanda ya Magharibi yenye makao yake mkoani Tabora, akisema hatua hiyo imeongeza kasi na ufanisi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya katika ukanda huo.

Sambamba na hilo, Kamishna Jenerali huyo ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Tabora kwa ushirikiano walioutoa katika operesheni hiyo, akibainisha kuwa bangi nyingi zinazolimwa mkoani humo hupandwa kwa siri katikati ya mapori na maeneo ya hifadhi.

“Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya hatutakubali uhalifu huu uendelee. Tutahakikisha tunafanya operesheni endelevu katika maeneo yote na kuchukua hatua za makusudi kwa watu wanaolima na kuzalisha dawa za kulevya ndani na nje ya mapori,” amesisitiza Lyimo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Paul Chacha, ameipongeza DCEA kwa juhudi kubwa inazoendelea kufanya katika kudhibiti dawa za kulevya mkoani humo, huku akitoa maelekezo kwa askari wa TFS kuweka kambi katika maeneo ya mapori na hifadhi ili kukomesha kabisa kilimo cha bangi kinachoendelea kufanyika kwa siri katika mkoa huo.

DCEA imesisitiza kuwa operesheni kama hizo zitaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini yenye viashiria vya uzalishaji wa dawa za kulevya, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kulinda afya ya jamii na kudhibiti vitendo vya kihalifu vinavyohusishwa na biashara hiyo haramu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img