15.6 C
New York

Biashara haramu ya dawa tiba za kulevya, kengele mpya ya tahadhari

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KUKAMATWA kwa chupa 1,795 za dawa tiba zenye asili ya kulevya katika basi la abiria lililokuwa likitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia mpaka wa Mutukula si tukio la kawaida. Ni ishara ya mwelekeo mpya wa mtandao wa mihadarati unaoanza kutumia mianya ya usafirishaji wa dawa halali za hospitali kama mbadala wa dawa za kulevya za viwandani.

Operesheni hiyo ya pamoja kati ya maafisa wa forodha na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilibaini maboksi 105 ya Pethidine, 31 ya Morphine Sulphate na 44 ya Fentanyl dawa zilizo katika kundi la opioids. Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, huu ni miongoni mwa ukamataji mkubwa kuwahi kutokea katika miaka ya karibuni.

“Zinapotoka katika mfumo rasmi wa tiba na kuingia mikononi mwa wasiostahili, hugeuka kuwa sumu hatari yenye uwezo mkubwa wa kusababisha uraibu na vifo,” ameeleza.

Kisheria, uingizaji na usambazaji wa dawa hizi unapaswa kufanywa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) pekee. Hivyo, kukamatwa kwake katika basi la abiria kunadhihirisha uwepo wa mtandao uliopangwa kuvuruga mfumo wa usambazaji wa dawa nchini na kanda ya Afrika Mashariki.

Wataalamu wa afya wanaonya kuwa ingawa opioids ni muhimu kupunguza maumivu makali kwa wagonjwa wa saratani au upasuaji, matumizi holela yanaweza kushusha pumzi, kuathiri fahamu na kusababisha kifo ndani ya muda mfupi.

Wakati huo huo, operesheni za kupambana na mihadarati zimeendelea kubaini tatizo sugu la bangi aina ya skanka na mirungi katika mikoa mbalimbali. Hali hii inaonyesha kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya bado ni ndefu na inahitaji ushirikiano wa kikanda, ufuatiliaji wa karibu wa mifumo ya dawa halali, pamoja na uelimishaji wa umma juu ya hatari zake.

Kwa mantiki hiyo, tukio la Mutukula ni zaidi ya ukamataji ni onyo kwamba mitandao ya mihadarati inabadilika mbinu, na mamlaka zinapaswa kuwa hatua moja mbele kila wakati.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img