KINSHASA, DRC
BARA la Afrika limepiga hatua kubwa tangu mwaka 2000 katika kukabiliana na vifo vya watoto wachanga, kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO).
Utafiti wa WHO umebaini kuwa kuanzia mwaka 2000 hadi 2023, vifo vya watoto wachanga vimepungua kwa asilimia 40, sawa na vifo 442 kutoka 727 katika kila watoto 100,000.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Shirika hilo, bado Afrika ina asilimia 70 ya vifo vya watoto wachanga duniani kote. Kwamba kila mwaka, Afrika hushuhudia vifo vya watoto milioni moja.
WHO inaeleza kuwa vifo vingi vinaepukika. “Katika maeneo mengi, ujauzito na kujifungua ni hatari inayoweza kusababisha kifo,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Afya la UN barani Afrika, Dkt. Chikwe Ihekweazu.
Mazingira yanayochagiza vifo hivyo, kwa mujibu wa WHO, ni pamoja na vita, magonjwa, uhaba wa wataalamu, na ubora mdogo wa vifaa-tiba.
Katika eneo la wataalamu, walau Afrika imeonekana pia kupiga hatua. Zaidi ya asilimia 80 ya huduma za kujifungua zinasimamiwa kwa weledi, tofauti na miaka mingi iliyopita, ambapo wanawake walijifungulia nyumbani.


