Na mwandishi wetu, Gazetini
KAMPENI nyingi zinazoendelea kwa sasa zimejikita kumpa nguvu mtoto wa kike/mwanamke. Jamii inampambania kweli kweli.
Wanaharakati wanafanya kila linalowekezana kumuweka binti/mwanamke katika nafasi wanayoamini anastahili. Jitihada ni kubwa mno.
Naweza kukubaliana nao katika eneo moja, kwamba ni kweli zipo baadhi ya jamii zilimkandamiza mwanamke na kumfanya aonekane kiumbe duni.
Katika baadhi ya maeneo, binti/mwanamke kumiliki mali ilitafsiriwa kuwa ni dhambi, kama si laana, achilia mbali kunyanyua sauti mbele ya mwanaume.
Haikujalisha sauti yake ingeibua maoni yenye fikra chanya au la. Hakuwa na haki ya kuzungumza, hata katika baadhi ya mambo yaliyomuumiza kimwili na kihisia.
Tunakubaliana, kwamba ni tamaduni dhaifu, ambazo zinazipa uhalali wa asilimia 100 kampeni zote za kumuinua mtoto wa kike/mwanamke.
Lakini, wakati huu wa harakati na kampeni nyingi za kumrudishia mwanamke hadhi yake, kuna mambo mawili jamii haipaswi kuyaacha nyuma. Ni yapi hayo? Twende taratibu.
Mosi, wanaojibebesha mabango ya usawa wa kijinsia hawapaswi kusahau kuwapa mabinti/wanawake elimu ya kutosha juu ya majukumu yao ya msingi.
Kwamba ‘usawa wa kijinsia’ haumaanishi kuwatoa kwenye majukumu yao ya asili, ambayo mara zote yanawataka kuwa chini ya mwongozo wa mwanaume.

Hicho kinachoitwa usawa hakimaanishi kuwa binti/mwanamke awe juu ya mwanaume, hasa katika mambo ambayo kimsingi yanamuhitaji kusikiliza na kufuata maelekezo.
Mathalan, katika ujenzi wa familia, asili inamtaka mwanaume kuwa ndiye kiongozi, licha ya kwamba hiyo haimpi nafasi ya moja kwa moja ya kusimika utawala wa kidikteta kwa mkewe au watoto.
Sasa, endapo tafsiri ya usawa wa kijinsia haitaeleweka vizuri, jamii itajikuta inazalisha ndoa ambazo wanawake wanakiuka asili kwa kutaka uongozi na kupaza sauti ndani ya familia.
Isivyo bahati, tafiti zinaweza kuthibitisha kuwa ni ndoa chache zilizofanikiwa kudumu kwa staili hiyo ya mwanaume kukubali kuwa msikilizaji, huku sauti ya mwisho ikitoka kwa mkewe.
Hivyo, ni lazima nguvu inayotumika kupigania usawa wa kijinsia pia iwe ya kiwango hicho hicho katika kuwaambia mabinti/wanawake kuwa bado asili inamtaka mwanaume kuhisi hadhi ya ufalme.
Inaweza isiwe na maana ya mwanaume kuwa na ‘final say’ (sauti ya mwisho) katika kila jambo, lakini hadhi yake inapaswa kubaki pale pale, hata wakati wa kukosolewa au kupewa wazo mbadala. Asili iko hivyo.
Hivi umewahi kujiuliza; kwanini wanaume huchagua wenza waliowazidi katika maeneo mengi, hasa wanapotaka kuoa? Mathalan, kijana msomi anaoa mwanamke asiyesoma au tajiri anaoa masikini?
Kimsingi, mwanaume huwa anatafuta nguvu ya asili. Mamlaka. Huhofia kuoa au kuingia kwenye mahusiano na msomi au tajiri mwenziye akikwepa kukosa mamlaka ndani ya nyumba. Iko hivyo.
Hivyo basi, wakati huu wa kampeni za usawa wa kijinsia, mabinti/wanawake wanapaswa kukumbushwa kuwa nguvu wanayopewa na wanaharakati haina uhusiano na kile wanachokitaka wanaume ndani ya nyumba.
Ikimaanisha, bado wanaume wanahitaji kupewa heshima, kusikilizwa na mamlaka. Hiyo ndiyo nguvu yao ya asili, ambayo ni ngumu kuondoshwa kwa kampeni.
Na kama itatokea mwanaume akaa za kuhisi, kusikia au kuona viashiria vya kupokonywa nguvu hiyo, basi aghalabu ndoa au uhusiano wa kimapenzi kati yake na mwanamke utakuwa umeishia hapo. Iko hivyo.
Pili, kwa jitihada kubwa zinazoendelea katika kumpambania binti/mwanamke, ambazo kimsingi zimeanza kufanikiwa, jamii ijiandae na vita ya kumuokoa mtoto wa kiume/mwanaume miaka 30 ijayo.
Kama ambavyo sasa inaonekana mabinti/wanawake wanahitaji kuokolewa, basi itakuwa hivyo pia kwa mtoto wa kiume/mwanaume.
Huenda ni kipindi ambacho mabinti/wanawake watakuwa washitakiwa wakubwa wa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.
Huenda ni kipindi ambacho tutashuhudia kesi zisizo na idadi za wanaume wanaokimbia ndoa kwa madai ya kupigwa na wake zao au kunyimwa unyumba.
Je, hawa tunaowaita ‘singel mothers’ waliojaa mitaani ni matokeo au kivuli cha picha halisi tutakayoiona kwa ukubwa wake kipindi hicho? Sijui.
Aidha, endapo jitihada za kumuinua kiuchumi mwanamke zitazaa matunda, basi hata kesi za wengi wao kushindwa kuhudumia familia (mume na watoto) nazo zinaweza kusikika kwa ukubwa wake wakati huo.
Ni kwa maana hiyo, wanaharakati wanaopambania usawa wa kijinsia kwa mabinti/wanawake wasimalize nguvu zote, na badala yake wabakize za kumsaidia mtoto wa kiume/mwanaume ifikapo 2056 au zaidi. Miaka 30 ijayo.
Kipindi ambacho jamii sasa italazimika kuwekeza nguvu kubwa katika kurejesha nguvu ya asili ya mtoto wa kiume/mwanaume iliyopotezwa na kampeni za kupigania binti/mwanamke.
Naomba kuwasilisha …


