10 C
New York

EAIF 2026 kufanyika kesho ikilenga kutoa fursa kwa vijana

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KONGAMANO la Uwekezaji Afrika Mashariki la mwaka 2026 (East Africa Investment Forum – EAIF 2026) linatarajiwa kufanyika kesho na kesho kutwa (Machi 26 na 27, 2026) jijini Dar es Salaam, likiwa jukwaa muhimu la kukuza uchumi wa kidijitali na kuwapa nafasi vijana wabunifu pamoja na wajasiriamali wa teknolojia kuonesha uwezo wao.

Kongamano hilo linatarajiwa kukutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya ukanda wa Afrika Mashariki, wakiwemo wawekezaji, wataalamu wa teknolojia ya fedha (fintech), watunga sera, wabunifu wa teknolojia na wajasiriamali. Lengo kuu ni kujadili mikakati ya kuharakisha ukuaji wa sekta ya kidijitali na kuongeza uwekezaji katika eneo hilo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 25, 2026, Katibu Mkuu wa Chama cha Watoa Huduma za Kifedha kwa Kutumia Teknolojia (Tafina), Shadrack Kamenya, amesema kongamano hilo litakuwa jukwaa mahsusi la kujadili sera, mazingira ya uwekezaji na changamoto zinazoikabili sekta ya fintech.

Amesema EAIF 2026 inalenga kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kubadilishana uzoefu, kujenga ushirikiano na kuweka mikakati madhubuti itakayowezesha ukuaji wa sekta ya teknolojia ya fedha pamoja na kuvutia uwekezaji zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Vodacom Tanzania, Buberwa Mukurasi, amesema ushiriki wa kampuni hiyo katika kongamano hilo unalenga kutoa nafasi kwa vijana kujifunza, kubadilishana mawazo na kuunganishwa na wawekezaji pamoja na wadau wa sekta ya teknolojia.

Amesisitiza kuwa vijana wana mchango mkubwa katika mapinduzi ya uchumi wa kidijitali, na kupitia EAIF 2026 watapata fursa ya kuonesha ubunifu wao, kujifunza kutoka kwa wataalamu wenye uzoefu mkubwa na kujenga mitandao itakayowasaidia kukuza biashara zao.

Kupitia majadiliano yatakayofanyika kesho na kesho kutwa, washiriki wanatarajia kubaini fursa mpya za uwekezaji, kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali, pamoja na kuweka mikakati itakayoongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi.

Aidha, kongamano hilo linatarajiwa kuwa chachu ya kuibua mawazo mapya ya kiteknolojia yatakayowawezesha vijana kujiajiri, kukuza biashara za kidijitali na kuongeza ajira katika uchumi unaoendelea kukua kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za robo ya mwaka 2025, hadi kufikia Septemba 2025, kampuni ya Vodacom Tanzania ilikuwa inamiliki asilimia 31.5 ya soko la mawasiliano ya simu nchini, jambo linaloonesha nafasi yake kubwa katika sekta ya mawasiliano na huduma za kidijitali.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img