Na mwandishi wetu, Gazetini
UTAFITI mpya wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) umebaini kuwa wagonjwa wapya wa saratani zaidi ya milioni saba wangeweza kuepuka ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa ripoti ya WHO, takribani asilimia 40 ya wagonjwa wapya wametokana na mazingira na mifumo ya maisha.
“Kwa sasa tunazo taarifa za namna ya kujiepusha na saratani kabla haijaanza,” anasema Isabelle Soerjomataram, mtaalamu wa Shirika la Kimataifa la Tafiti za Saratani (IARC).
Soerjomataram anasema unafiti wao uliochapishwa katika Jarida la Nature Medicine umehusisha mataifa 185 na kugusa aina 36 ya saratani.
“Asilimia 37.8 ya wagonjwa wapya wa saratani, ambao ni takribani milioni 7.1 kwa mwaka 2022 wametokana na matumizi ya tumbaku na pombe,” anasema.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa tafiti kuonesha uhusiano uliopo kati ya saratani na mazingira au mifumo ya maisha.
Zipo tafiti nyingi zinazotaja unene uliopindukia (obesity), hewa chafu, uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kuwa ni visababishi vya ugonjwa huo.


