Na mwandishi wetu, Gazetini
ILI kuongeza uelewa wa sheria za ushindani na taratibu za rufaa katika shughuli za kibiashara, Fair Competition Tribunal (FCT) imewakutanisha wafanyabiashara na walaji wa Mkoa wa Lindi katika mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo kuhusu ushindani wa haki na mfumo wa rufaa.
Akizungumza Jumatatu, Machi 2, 2026 kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Katibu Tawala Msaidizi (Utawala na Rasilimali Watu), Nathalis Linuma, amesema mafunzo hayo yatawasaidia wadau kuelewa namna sheria na kanuni za ushindani zinavyofanya kazi pamoja na nafasi ya FCT katika kusikiliza na kutatua migogoro ya kibiashara.

“Mafunzo haya yatakwenda kuwa chachu kwenu kwa kuongeza uzalishaji na kupunguza migogoro ya kibiashara,” amesema Linuma.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Baraza la Ushindani, Kunda Mkenda, amesema mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu kuhusu mfumo wa rufaa unaotumika pale kunapotokea malalamiko yanayohusiana na mwenendo usio wa haki sokoni, ikiwemo katika sekta za miundombinu na huduma nyingine za kibiashara.
“Baraza la Ushindani lina jukumu la kusikiliza na kutatua migogoro inayotokana na mienendo isiyo ya haki katika soko kupitia mfumo wa rufaa,” amesema Mkenda.
Naye Ofisa Tehama wa FCT, Athumani Juma, amesema taasisi hiyo imejikita katika matumizi ya teknolojia kurahisisha upatikanaji wa haki, ikiwemo kufungua kesi za rufaa kwa njia ya mtandao.
Mmoja wa washiriki, Angel Kessy, amesema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa haki na wajibu wao, hatua itakayochangia kupunguza migogoro na kuimarisha ushindani wenye tija.


