Na Christopher Cyrillo
KIM Jong- nam, mtoto wa kwanza wa Kim Jong – il alitazamwa kama mrithi wa utawala wa Korea Kaskazini baada ya kumalizika kwa utawala wa baba yake.
Mwaka 2001 alikamatwa nchini Japan kwa kosa la kutumia hati bandia ya kusafiria, akijiita kwa jina la kichina Pang Xiong.
Kukamatwa kwake kulimchukiza baba yake ambaye alianza kumuona hafai kurithi utawala wa Korea Kaskazini kwa sababu ya kushindwa kutumia mbinu nyepesi ya kughushi hati ya kusafiria. Mwaka 2003, Kim Jong-alitoroka nchini Korea kaskazini na kwenda kujificha huko Macau-China.
Mamlaka za Korea Kaskazini zilimbatiza jina la uasi kutokana na utaratibu wake wa kukosoa utawala wa Baba yake kwenye vyombo vya habari vya kimataifa.
Septemba 2010, mtoto mdogo wa familia ya uongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un alipangwa kuwa mrithi wa uongozi wa nchi hiyo.
Majasusi wa CIA waliamua kumtumia Kim Jong – nam kwa ajili ya kupata taarifa za Korea Kaskazini na ikibidi wamuandae kushika madaraka ya nchi hiyo kwa kumpindua Kim Jong- un.
Desemba 2011, Kim Jonh- un alishitukia mpango wa kumpindua uliosukwa na mjomba wake, wenye lengo la kumrudisha Kim Jong –nam nchini Korea Kaskazini ili aongoze nchi hiyo. Baada ya kushitukia mpango huo, mjomba aliuawa.
Februari 2017, Kim Jong – nam alionekana kwenye viyunga vya uwanjwa wa ndege mjini Kuala Lumpur akitazamiwa kusafiri kurudi Macau, lakini masaa mawili baadaye aliaga dunia.
Sumu aina ya VX ndiyo iliyotumiwa na majasusi wa Korea Kaskazini waliokuwapo uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur, kwa kazi maalum ya kumuua mpinzani wa utawala wa Kim Jong – un. Wasichana wawili, Siti Aisyah, raia wa Indonesia na Doan Thi Huong wa Vietnam walitumiwa bila kujua.
Wanaume wanne waliosafiri kutoka Korea Kaskazini waliwakabidhi wasichana hao manukato ya kupuliza na kuwasihi wasijipulizie wao bali wampulizie Kim Jong – nam kana kwamba ni mchezo wa kuigiza ambao huchukuliwa video kwa siri na baadaye wahusika wote na watu wengine huangalia video hiyo na kucheka pamoja.
Wasichana waliaminishwa kuwa tukio hilo litamfurahisha Mr. Kim kwani ilikuwa siku yake ya kuzaliwa, na wao watafurahi pia kushiriki mchezo huo. Hawakujua manukato yale si manukato bali ni moja kati ya sumu kali maalum kwa kuita mauti.
Lakini kabla ya wasichana wale kumpulizia manukato Mr. Kim (Kim Jong – nam) hakuonekana mvulana hata mmoja miongoni mwa wale waliowalaghai akina Siti na Huong, walitoweka kusikojulikana.
Wasichana walikamatwa kwa tuhuma za kumuua Kim Jong-nam, lakini baadaye walifutiwa mashitaka ya mauaji baada ya vyombo vya usalama vya nchini Malaysia kujiridhisha kuwa walitumiwa bila kujua.
Mwandishi ni mchambuzi mahiri na mbobezi wa masuala ya kijamii na kisiasa.


