Na mwandishi wetu, Gazetini
MATAIFA mawili yanayopeana upinzani mkali katika nyanja ya kiuchumi, yakitajwa kuongoza duniani kwa upande wa maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kupitia utafiti wake, tovuti ya Visual Capitalist imefanya utafiti wa gharama za maisha katika mataifa hayo, ukiangazia bei ya bidhaa na huduma muhimu za kila siku.
Katika utafiti huo, China imeonekana kuwa na urahisi wa maisha kutokana na unafuu wa maisha, ukilinganisha na Marekani.
Mathalan, wastani wa kodi ya chumba kimoja cha kulala maeneo ya mjini kwa China ni Dola 559, wakati kwa Marekani ni Dola 1,747.
Kama ni nyumba ya wastani, kodi hufikia Dola 52 kwa mwezi nchini China, ikiwa ni pamoja na gharama za umeme na takataka. Kwa Marekani, inagharimu Dola 210.
Wakati huo huo, wastani wa bei ya chakula katika mgahawa wa kawaida nchini China ni Dola 2.84, huku kwa Marekani ikiwa ni Dola 20.
Hata kwa upande wa migahawa ya kifahari, bado pia China ina unafuu. Mathalan, wastani wa bei ya chakula katika Mgahawa wa McDonald nchini China ni Dola 4.97, wakati kwa Marekani ni Dola 12.
Kwa China, kama hiyo haitoshi, wastani wa bei ya mayai (trei moja) ni Dola 1.57, wakati ni Dola 4.41 kwa Marekani.
Pia, chupa moja ya pombe kwa China ni wastani wa Dola 11.36, wakati huo ikiwa ni Dola 15 kwa upande wa Marekani.
Kama hiyo haitoshi, wastani wa bei ya tiketi ya muvi, mathalan katika ukumbi wa sinema, ni Dola 6.39 tu, tofauti na Marekani, ambako ni Dola 15.
Aidha, wastani wa gharama za chini za intaneti kwa mwezi nchini China ni Dola 11, wakati huo ni Dola 72 kwa Marekani.
Je, tofauti kubwa ya gharama za maisha kati ya China na Marekani inatokana na nini? Ni ruzuku ya Serikali ya China katika baadhi ya bidhaa, pia unafuu wa gharama za nishati.


