DUBAI, UAE
UMOJA wa Falme za Kiarabu (UAE) umechangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 20 kwa ajili ya chakula nchini Sudan, ambako vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekita mizizi.
Msaada huo wa fedha ni sehemu ya ushirikiano uliopo kati ya UAE na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP).
Kwa sasa, Sudan iko kwenye hali ya usalama kutokana na mapigano ya wanajeshi wa Serikali, SAF, na wale wa RSF, chanzo cha mgogoro kikiwa ni kugombea madaraka ya kuiongoza nchi hiyo.
Jumuhiya ya kimataifa, wakiwamo pia wanaharakati wa haki za binadamu, wamekuwa wakizishutumu pande zote mbili na kuzitaja kuhusika katika uhalifu wa kivita.
“Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa unapenda kuushukuru Umoja wa Falme za Kiarabu kwa mchango wake wa dhati wa Dola milioni 20, ambao utatusaidia kuokoa maisha huko Sudan,” inaeleza taarifa ya WFP.


