Na mwandishi wetu, Gazetini
‘BANANA’, kama inavyotamkwa kwa Kiingereza, ni neno lenye maana ya ‘ndizi’ kwa tafsiri ya lugha ya Kiswahili.
Katika duru za kisiasa, ‘Banana Republic’, kama wengine wanavyoweza kuita ‘Jamhuri ya Ndizi’, ni msamiati maarufu, ingawa kwa wengine (wasio wachambuzi/wafuatiliaji wa siasa) unaweza kuwa mpya kwao.
Turudi na kuchimbua kidogo katika historia. Nini chimbuko la neno hilo? Tujue; lilianzia wapi? Nani muasisi wake? Endelea kusoma …
Neno ‘Jamhuri ya Ndizi lilianza kutumiwa na mwandishi wa vitabu maarufu wa Marekani, O. Henry, ambaye jina lake halisi ni William Sydney Porter.

Historia inatumbukusha kuwa O. Henry alikimbia Marekani na kutimkia Honduras mwaka 1896, akikwepa mashitaka ya ufisadi aliyokuwa amefunguliwa na Benki ya Texas.
Akiwa Honduras, O. Henry aligundua jambo kuhusu kampuni kubwa mbili za mazao ya ndizi za Marekani alizozikuta nchini humo.
Alionao nini? O. Henry aligundua kuwa viongozi wa kampuni hizo walikuwa wameushika mfumo wa siasa za Honduras na kuifanya Serikali ya nchi hiyo iwe butu na isiyo na sauti mbele yao.
Kwa lugha rahisi, wao ndiyo walioamua nani awe kiongozi, nani anapaswa kubambikiziwa kesi, nani anastahili kupewa au kunyimwa haki, na ni sheria zipi zinafaa kuongoza raia.
Kwa kutazama maisha hayo, ndipo mwandishi huyo alipopata wazo na kuandika riwaya yake ya kusadikika ya ‘Cabbages and Kings’ mwaka 1904.
Katika riwaya hiyo, akichukua picha ya Honduras na kampuni za mazao ya ndizi za Marekani, O. Henry alisema ‘Jamhuri ya Ndizi’ ni serikali yoyote ile inayolinda masilahi ya wageni, huku wazawa (raia) wakiwa hawana tumaini.
“Ni kuanzia hapo, wasomi, waandishi wa habari, wanasiasa na waandishi wa vitabu wakaaanza kutumia neno ‘Jamhuri ya Ndizi’ kuitaka Serikali iliyotawaliwa na rushwa na kushindwa kujiendesha,” anasema Carlos Dada, ambaye ni Mkurugenzi wa Gazeti la El Faro la Salvador.
Salvador, ambaye ni mwandishi nguli wa habari za uchunguzi, anasema mfano halisi wa miaka ya zamani wa ‘Jamhuri ya Ndizi’ ni mataifa manne ya Amerika; Honduras, Guatemala, Nicaragua na Costa Rica.
Msomi huyo anatolea mfano namna kampuni za mazao ya ndizi za Marekani, United Fruit Company (UFC) na Standard Fruit, zilivyokuwa zikitawala serikali za nchi hizo.
Je, Serikali za Afrika zinakwepa kwa namna gani kuingia na kuchorwa kama kielelezo cha ‘Banana Republic’? Makala haya yanachokoza na kufungua uwanja mpana wa mjadala.


