Na mwandishi wetu, Gazetini
WIZARA ya Madini imetangaza mafanikio makubwa katika utekelezaji wa ahadi na maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100 za awamu ya pili ya uongozi wake katika Awamu ya Sita, yakihusisha ongezeko la makusanyo ya maduhuli, mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa (GDP), uongezaji thamani wa madini na ushiriki mpana wa Watanzania katika shughuli za uchimbaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Januari 26, 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema taarifa hiyo imejikita katika maeneo 10 muhimu yanayochangia moja kwa moja ukuaji wa sekta ya madini na ustawi wa wananchi.
Makusanyo ya maduhuli yapaa kwa kasi
Mavunde amesema makusanyo ya maduhuli katika sekta ya madini yameongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka Sh bilioni 213.36 mwaka wa fedha 2016/2017 hadi kufikia Sh trilioni 1.07 mwaka 2024/2025, sawa na asilimia 107.13 ya lengo lililowekwa la kukusanya Sh bilioni 999.99.
“Mafanikio haya yametokana na marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 pamoja na usimamizi thabiti wa rasilimali madini kwa manufaa ya taifa,” amesema Mavunde.
Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, wizara ilikusanya Sh bilioni 653.94 sawa na asilimia 108.99 ya lengo la kipindi hicho, ikiwa ni asilimia 54.43 ya lengo la mwaka mzima wa fedha 2025/2026 la kukusanya Sh trilioni 1.2. Aidha, kati ya Novemba 2025 hadi Januari 25, 2026, Sh bilioni 311.80 zilikusanywa, sawa na asilimia 111 ya lengo.
Mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa waongezeka
Kwa mujibu wa Mavunde, mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024. Aidha, katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 mchango huo ulifikia asilimia 11 na kuongezeka hadi asilimia 12 katika robo ya pili ya mwaka huo.
Serikali yaongeza thamani ya madini
Katika eneo la uongezaji thamani, wizara inaendelea kukamilisha Mkakati wa Uongezaji Thamani Madini wa miaka mitano kuanzia 2026/2027 hadi 2030/2031, ambapo viwanda vitajengwa katika mikoa sita ya kimadini ikiwemo Arusha, Dodoma, Kahama, Mbeya, Lindi na Pwani.
Mavunde alisema ujenzi wa jengo la Ofisi za Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) jijini Arusha unaendelea kwa gharama ya Sh bilioni 33 na umefikia asilimia 10 ya utekelezaji. Aidha, kati ya Julai hadi Desemba 2025, tani 14.66 za dhahabu zenye thamani ya Sh trilioni 3.75 ziliuzwa kwenye viwanda vya kusafisha dhahabu vilivyopo nchini.
“Hadi Desemba 2025, Benki Kuu ya Tanzania imeongeza akiba ya dhahabu kwa kununua tani 17.03 zenye thamani ya Sh trilioni 4.97,” amesema.
Ushiriki wa Watanzania waongezeka
Mavunde alieleza kuwa ajira kwa Watanzania katika migodi zimeongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2018 hadi asilimia 97 mwaka 2024. Vilevile, manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni za Kitanzania yameongezeka hadi asilimia 88 mwaka 2024 kutoka asilimia 62 mwaka 2018.
Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, asilimia 99.41 ya manunuzi ya migodi yalifanywa kupitia kampuni za Kitanzania.
Leseni, masoko na uwazi wa biashara
Wizara imetoa jumla ya leseni 12,130 mwaka wa fedha 2024/2025 sawa na asilimia 117.8 ya lengo. Aidha, masoko 44 ya madini na vituo 117 vya ununuzi vimeendesha biashara ya madini yenye thamani ya Shilingi trilioni 3.102 kati ya Julai na Desemba 2025.
Maabara, minada na nishati safi
Serikali imeanza ujenzi wa maabara kubwa ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini Kizota, Dodoma kwa gharama ya Sh bilioni 14.3. Pia, minada mitatu ya madini ya vito imefanyika na kuingiza zaidi ya Sh bilioni 247 kwa Serikali.
Katika sekta ya nishati safi, wizara imenunua mitambo ya Rafiki Coal Briquettes itakayozalisha nishati mbadala rafiki kwa mazingira katika mikoa ya Dodoma na Tabora.
Utafiti wa madini waimarishwa
Serikali imeongeza eneo lililofanyiwa utafiti wa jiolojia katika Wilaya za Kibiti na Rufiji hadi asilimia 98 na kusimikwa vituo 32 vya kufuatilia mitetemo ya ardhi.
Kwa ujumla, Mavunde alisema mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha rasilimali madini zinatumika kama injini ya maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi.


