10.1 C
New York

OWM yakabidhi msaada kwa waathirika wa mafuriko Kilosa

Published:

KILOSA, Morogoro

OFISI ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa, leo Januari 2, 2026, imekabidhi vifaa mbalimbali vya misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa mafuriko katika Kata ya Tindiga, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.

Makabidhiano ya misaada hiyo yamefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa na kuongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. James Kilabuko, akishirikiana na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Brigedia Jenerali Hosea Ndagala.

Misaada hiyo imepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mheshimiwa Shaka Hamdu Shaka, akiwa ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na magodoro 90, vyandarua 90, mablanketi 90, mahema matano pamoja na ndoo 90 kwa ajili ya kaya zilizoathirika. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa msaada wa chakula unaojumuisha unga tani 7.2, maharage tani 2.1, mafuta ya kupikia lita 360, chumvi kilo 300 na sukari kilo 600.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Dk. Kilabuko amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za haraka kuhakikisha waathirika wa maafa wanapata msaada wa msingi, huku akisisitiza ushirikiano wa karibu kati ya serikali kuu na mamlaka za wilaya katika kukabiliana na athari za majanga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ameishukuru Serikali kwa msaada huo, akibainisha kuwa utapunguza changamoto zinazowakabili wananchi waliopoteza makazi na mali zao kutokana na mafuriko.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img