8.4 C
New York

Mambo 5 kuhusu kocha mpya Simba

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

HATIMAYE ni Steve Barker ndiye aliyetangazwa kuwa kocha mkuu mpya wa Simba akichukua mikoba ya Dimitar Pantev aliyefungashiwa virago wiki chache zilizopita.

Barker ni nani? Kupitia makala haya, GAZETINI inakuibulia mambo matano (5) usiyoyajua kuhusu kocha huyo raia wa Afrika Kusini. Endelea kusoma.

Familia ya soka

Barker (57), anatokea familia yenye heshima kubwa katika mchezo wa soka nchini Afrika Kusini. Ni mtoto wa dada (mpwa) wa kocha wa zamani wa timu ya taifa ‘Bafana Bafana’, Clive Barker.

Historia ya soka la Afrika Kusini inakumbuka kuwa Clive ndiye aliyekuwa kocha wakati Bafana Bafana ilipotwaa ubingwa wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) za mwaka 1996. Kwa upande wake, Barker naye aliwahi kucheza soka. Ni kiungo wa zamani wa klabu za Wits University na SuperSport United.

Lakini, alianza kazi ya ukocha mwaka 2008 akiwa na timu ya Chuo Kikuu cha Pretoria, ambayo aliinoa kwa miaka sita. Mwaka 2014, alijiunga na Amazulu na kufanya nayo kazi kwa miaka miwili, kabla ya kuajiriwa na Stellenbosch mwaka 2017.

Miaka tisa ya mafanikio

Barker amejiunga na Simba baada ya miaka tisa ya mafanikio makubwa akiwa na Stellenbosch FC ya Ligi Kuu nchini Afrika Kusini.

Heshima kubwa aliyonayo mbele ya mashabiki wa Stellenbosch ni namna alivyoitoa timu hiyo Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu (Betway Premiership).

Kama hiyo haitoshi, Barker aliiongoza Stellenbosch FC kutwaa ubingwa wa michuano ya Carling Knockout mwaka 2023, pia wakifika mara mbili fainali ya Kombe la Ligi (MTN8).

Si tu kufika mafanikio hayo, bali pia huu ni msimu wa pili mfululizo kwa kocha huyo kuiwezesha timu yake hiyo kucheza michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akutana na Simba kimataifa

Ni msimu uliopita wa Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo Stellenbosch ya Barker ilikutana na Simba katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya CAF (Shirikisho la Soka Afrika).

Itakumbukwa, Simba ilisonga mbele na hatimaye kukutana na RS Berkane katika mchezo wa fainali. Vigogo hao wa Morocco waliibuka na ushindi na kutwaa ubingwa.

Upepo mbaya msimu huu (2025-26)

Msimu huu haijawa mzuri kwa Barker katika klabu ya Stellenbosch. Ameondoka ikiwa nafasi za chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Katika mechi zao 14, wameshinda tatu, sare tatu na kufungwa nane, huku ikiwa ni pointi moja pekee inayowatenganisha na mstari wa kushuka Daraja.

Mbali ya kupoteza fainali ya Kombe la Ligi (MTN8), pia waliishia robo fainali ya michuano ya Carling Knockout kwa kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Marumo Gallants.

Hata lawama zitaelekea kwa mabosi wa klabu hiyo kwa kuwapoteza wachezaji wengi muhimu waliotimkia kwa wapinzani wao.

Miongoni mwao ni Ashley Du Preez na Zitha Kwinika waliojiunga na Kaizer Chiefs, Jayden Adams (Mamelodi Sundowns) na Deano van Rooyen na Sihle Nduli (Orlando Pirates).

Changamoto yake Simba

Barker anaikuta Simba ikiwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni michuano mipya kwake kwani uzoefu wake wa misimu miwili ni kwenye Kombe la Shirikisho.

Pia, Barker anaikuta Simba ikiwa imeshapoteza mechi zote mbili za Kundi D msimu huu wa Ligi ya Mabingwa. Kwamba ana mechi sita za kuiwezesha kuvuka makundi na kuingia hatua ya 16 Bora.

Kabla ya ujio wa Pantev, raia mwenzake wa Afrika Kusini, Fadlu Davis, aliiwezesha Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Wakati huo huo, ‘Wekundu wa Msimbazi’ wako nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara. Katika mechi zake tano, wameshinda nne na kufungwa moja.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img