Na mwandishi wetu, Gazetini
WAPO waliozoea kulala wakiwa wamewasha taa zao za ndani nyakati za usiku, bila kufahamu kuwa inaweza kuwasabashia shambulio la moyo au ugonjwa wa kiharusi.
Hayo yameibuliwa na Chama cha Madaktari wa Ugonjwa wa Moyo nchini Marekani (AHA) katika utafiti wake wa hivi karibuni.
Katika utafiti wao uliofanyika kwa miaka 10, wataalamu hao walibaini kuwa mwanga wa taa kwa mtu aliyelala nyakati za usiku huathiri utendaji kazi wa ubongo.
Hivyo, kwa mtu mwenye kawaida ya kulala na taa, ana asilimia 35 ya kupata shambulio la moyo baada ya miaka mitano tu na asilimia 22 ya kuumwa kiharusi baada ya miaka 10.
Ni utafiti ulihusisha watu 466, ambao wastani wa umri wao ulikuwa ni miaka 55, huku asilimia 43 wakiwa ni wanaume.
Kabla ya kuingizwa katika utafiti wa miaka 10, walifanyiwa vipimo kubaini hali ya afya zao, ambapo majibu yalionesha kuwa hakukuwa na mwenye tatizo la moyo au saratani.
Ni baada ya majibu ya utafiti kuonesha kuwa waliokuwa wakilala na taa nyakati za usiku wamepata shambulio la moyo na kiharusi, wataalamu wa AHA wanashauri kuwa ni vizuri kuepuka tabia hiyo.
Pia, katika ripoti yao, AHA wanashauri kuwa ni vizuri kulala nyakati za usiku katika chumba chenye giza ili kuepuka hatari zilizoelezwa.
“Giza hupoza mwili, ikiwamo kupunguza shinikizo la damu. Kwa kadiri mwanga unavyokuwa mwingi usiku, ndipo shinikizo la damu linavyochelewa kupunguza,” anasema Jayne Morgan, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya moyo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Hello Heart.

Kwa upande mwingine, utafiti wa AHA haupishani kimatokeo na ule wa mwaka 2022 uliowagawa washiriki katika makundi matatu.
Kundi la kwanza lilitakiwa kulala katika chumba chenye giza kabisa. Kundi la pili lilielekezwa kulala chumba chenye mwanga hafifu. Kundi la tatu lililala katika chumba chenye mwanga kamili.
Matokeo ya utafiti yalionesha kuwa washiriki wa kundi la tatu, ambao walilala kwenye mwanga mwingi, waliamka na kukiri kuwa mapigo ya moyo yameongezeka.


