5.7 C
New York

Usiyoyajua kuhusu ugonjwa uliomuua Tagawa; dereva aliyetikisa soko la filamu

Published:

TOKYO, Japan

WAPENZI wa filamu za mapigano walimfahamu zaidi kwa ukatili wake katika ‘muvi’ alizoigiza kama ‘kubwa la maadui’, ikiwamo ‘Mortal Kombat’. Huyo ndiye anaitwa Cary-Hiroyuki Tagawa.

Mwigizaji huyo mzaliwa wa Tokyo, Japan, alifariki hivi karibuni akiwa na umri wa miaka 75, taarifa iliyotikisa soko la filamu duniani kote.

Hadi anakutwa na umauti, Tagawa alikuwa kitandani akiwa amezungukwa na familia yake huko California.
Akitangaza kifo chake, aliyekuwa meneja wake, Margie Weiner, alisema: “Kumpoteza ni taarifa ambayo haielezeki kwa uzito wake. Moyo wangu uko na familia, marafiki na wote waliompenda.”

“Najivunia kuwa meneja wa Cary-Hiroyuki Tagawa kwa miaka mingi, lakini uhusiano wetu ulienda mbali zaidi na kuwa familia.”

CHANZO CHA KIFO CHAKE

Nini kilichokatisha maisha ya mwamba huyo? Kwa mujibu wa meneja wake, Weiner, chanzo cha kifo cha Tagawa ni ugonjwa wa kupooza.

Wataalamu wa afya wanasema ugonjwa huo hutokana na damu kushindwa kufika au kufika kwa kiwango kidogo katika ubongo. Hiyo husababisha tishu za ubongo kukosa hewa ya oksijeni.

Takwimu ziko wazi, kwamba ripoti zinaeleza kuwa ugonjwa huo huwapata watu zaidi ya 795,000 kila mwaka nchini Marekani.

Katika hatua nyingine, ripoti ya mwaka 2022 inaonesha kuwa kati ya vifo sita nchini Marekani, kimoja hutokana na ugonjwa huo.

SAFARI, MAFANIKIO YAKE

Tagawa alianza kuigiza akiwa na umri wa miaka 36 baada ya kufanya kazi mbalimbali, ikiwamo ya udereva katika kampuni ya kusambaza ‘pizza’.

Hata hivyo, umaarufu alionao leo hii kwenye tasnia ya burudani ulianza mwaka 1987, apoonekana kupitia filamu ya ‘The Last Emperor’, ambayo ilifanya vizuri na kutwaa tuzo ya Oscar.

Ni baada ya hapo, Tagawa akaanza kufahamika na kuonekana katika filamu nyingi, zikiwamo ‘Pearl Harbor’, ‘Planet of the Apes’ na ‘License to Kill’.

BABA MWANAJESHI, MAMA MWIGIZAJI

Baba yake ni mzaliwa wa Hawaii, Marekani, ambaye pia aliwahi kuhudumu katika jeshi la nchi hiyo miaka mingi iliyopita.

Akiwa kwenye majukumu ya kazi nchini Japan, ndipo mzee huyo alipokutana na mwanamke aitwaye Ayako, ambapo walianzisha mahusiano yaliopelekea kuzaliwa kwa Tagawa.

Wakati huo na hata baada ya ndoa, Ayako alikuwa mwigizaji wa tamthilia za majukwaani mwenye umaarufu wa wastani nchini Japan.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img