Na mwandishi wetu, Gazetini
KATIKA ajali ya basi lililowaka moto, abiria 40 waliokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Malinyi, Morogoro, wamenusurika kupoteza maisha. Ni baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuteketea kwa moto eneo la Maseyu, tukio lililotokea leo Desemba 9, 2025, katika kona ya Maseyu, Kata ya Gwata.
Taarifa zinaeleza kuwa basi hilo aina ya Tata lilianza kuwaka moto, ingawa abiria walifanikiwa kutoka wakiwa hawajajeruhiwa.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva Halfan Omary, mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam.
“Hili gari limeteketea kabisa, lakini tunashukuru hakuna abiria aliyejeruhiwa. Hata hivyo, mizigo na mali nyingine za abiria zilizokuwamo ndani zimeungua,” amesema Kamanda Mkama.
Akifafanua zaidi, Kamanda Mkama amesema chunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya mfumo wa umeme wa gari.
Aidha, ametoa wito kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri kuhakikisha magari yao yanakaguliwa na kufanyiwa matengenezo ili kuepusha ajali za aina hiyo.


