Na Hassan Mwasha, Gazetini
NI Jumapili ya wiki hii, ambapo Simba watakuwa wenyeji wa matajiri wa Chamazi, Azam FC, ukiwa ni mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu wa 2025-26. Azam watashuka dimbani wikiendi hii wakiwa na hamu ya kulipa kisasi kwani mara yao ya mwisho kupata ushindi mbele ya Simba ni Oktoba 27, 2022, ambapo wakiwa Azam Complex walishinda bao 1-0.
Takwimu zikoje?
Kuelekea mchezo huo maarufu kwa jina la ‘Mzizima derby’, Simba wameshacheza mechi nne na kukusanya pointi 12 na wanashika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Bara. Katika michezo mitano hiyo, wakali hao wa Kariakoo wamefunga mabao 11, huku safu ya ulinzi ikiwa imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara moja pekee.
Simba watarejea dimbani wakiwa na ‘mzuka’ baada ya ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo uliopita. Kwa upande wao, Azam chini ya kocha raia wa DRC, Florent Ibenge, wamekusanya pointi sita katika mechi zao nne walizoshuka dimbani msimu huu.
Mechi zao nne zimeishuhudia Azam ikiwa na mabao matano ya kufunga, licha ya kwamba pia imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne. Matajiri hao wa Chamazi wataikabili Simba wakiwa na machungu ya kulazimishwa suluhu (0-0) wakiwa nyumbani katika mchezo uliopita dhidi ya Singida Black Stars.
Hasira zinaanzia CAF
Timu hizo za jijini Dar es Salaam zinakutana wakati huu kila moja ikiwa na hasira za kufanya vibaya msimu huu wa michuano ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (CAF).
Ikumbukwe, Simba imepoteza mechi zote mbili za hatua ya makundi msimu huu wa Ligi ya Mabingwa, ambapo ilifungwa na Petro de Luanda (nyumbani, 1-0) na Stade Malien (ugenini, 2-1).
Azam, kwa upande wao, nao wamefungwa mechi zote mbili za Kombe la Shirikisho Afrika, walifungwa na Maniema Union (ugenini 2-0) na Wydad Casablanca (nyumbani, 1-0).
Rekozi zinasemaje?
Hii itakuwa mara ya 34 kwa Simba na Azam kukutana. Katika michezo 33 iliyopita, Wekundu wa Msimbazi wameshinda 14, Azam wametamba mara 8, huku sare 11 zikijitokeza.
Mechi ya mwisho kuikutanisha miamba hiyo ni ile ya Februari 24, mwaka huu, ambayo Simba ilikuwa mwenyeji na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.


