TUNIS, Tunisia
MWANASIASA maarufu wa upinzani nchini Tunisia, Ayachi Hammami, amekamatwa na polisi ili kwenda kutumikia kifungo cha miaka mitano gerezani.
Hammami ni miongoni mwa wanasiasa wa upinzani, akiwamo Chaima Issa, waliohukumiwa kwa makosa ya uhaini, wakitajwa kusuka mpango wa kuipindua Serikali ya Rais Kais Saied.
Hata hivyo, kwa mtazamo wa wakosoaji wake, hukumu hiyo kwa wapinzani ni mwendelezo wa utawala wa kidikteta wa Rais huyo.
Kwa upande wake, Hammami aliwahi kuwa Waziri wa Haki za Binadamu nchini Tunisia mwaka 2020.
Katika video aliyoposti mitandaoni muda mfupi kabla ya kukamatwa, alisema: “Nimetumia miaka mingi kupigania Demokrasia, uhuru na haki. Nitageuza chumba changu cha gereza kuwa mwanzo mpya wa mapambano.”
Aidha, wakosoaji wanaongeza kuwa hukumu yake ni mwendelezo wa Mahakama kutumika kulinda masilahi ya Serikali iliyoko madarakani.


