PRETORIA, Afrika Kusini
AFRIKA, kama ilivyo kwa mabara mengine duniani, imeendelea kuwekeza katika elimu ya juu, ikishuhudia mamilioni ya wahitimu wa vyuo vikuu wakiingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Times Higher Education (THE), ambayo hufanya tathmini ya ubora wa vyuo katika nchi 115 duniani, Misri na Morocco zimeendelea kuwa na vyuo vikuu bora Afrika.
Wakati huo huo, Afrika Kusini inaongoza kwa uwekezaji wa elimu ya juu, ambapo kati ya vyuo vikuu bora 11 barani Afrika, saba vinapatikana katika Taifa hilo lililopata uhuru wake mwaka 1994.
Chuo Kikuu bora zaidi, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu, ni Cape Town (UCT), ambacho kina wafanyakazi zaidi ya 5,000 na wanafunzi 29,000 kutoka mataifa zaidi ya 100.
Chuo Kikuu cha Stellenbosch kinashika nafasi ya pili kwa ubora barani Afrika. Taasisi hiyo ya elimu ya juu ilianzishwa mwaka 1981 kikiwa na wanafunzi 503 na wahadhiri 40 pekee.
Leo hii, Chuo hicho kimejitanua zaidi katika ardhi ya Afrika Kusini, ambapo kina wanafunzi 32,225 na wafanyakazi 3,400.
Nafasi ya tatu inashikwa na Chuo Kikuu cha Witwatersrand cha Afrika Kusini. ‘Wits’, ambacho kilianzishwa mwaka 1986, kikitokea katika iliyokuwa ikiitwa Shule ya Madini ya Afrika Kusini.
Chuo Kikuu cha Mohamed VI kinafuata katika nafasi ya nne. Kilianzishwa mwaka 2016 na kinapatikana mjini Benguerir, Morocco.
Kutokana na uwekezaji mkubwa wa teknolojia, Chuo hicho kimekuwa moja ya vituo muhimu vya tafiti barani Afrika.
Pia, kipo Chuo Kikuu cha Johannesburg cha Afrika Kusini. Miongoni mwa fani zinazotolewa chuoni hapo ni Sayansi ya Afya, Sheria, Uhandisi na Biashara na Uchumi.
Ubora wake unakifanya Chuo Kikuu hicho kuwavutia wanafunzi na wafanyakazi kutoka mataifa zaidi ya 50 barani Afrika.
Chuo kingine bora barani Afrika, kwa mujibu wa Taasisi ya Times Higher Education (THE), ni Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia nchini Misri (E-JUST).
Chuo hicho kilianzishwa mwaka 2009 kwa ushirikiano wa Misri na Serikali ya Japan na kinapatikana mjini Alexandria.
Nafasi ya saba inashikwa na Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal cha Afrika Kusini. Kilianzishwa mwaka 2004 baada ya vyuo vikuu viwili, Durban-Westville na Natal, kuungana.
Chuo Kikuu cha Amerika mjini Cairo kilichoanzishwa mwaka 1919 kinashika nafasi ya nane, kikifuatiwa na Chuo Kikuu cha Future (2006) na Chuo Kikuu cha Kafrelsheikh (2006), vyote vikiwa nchini Misri.
Published:


