Na Mwandishi Wetu, Gazetini
MKURUGENZI wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, amewataka washiriki wa Jukwaa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni juu ya rasimu ya Mpango wa Taifa wa Dharura wa kukabiliana na ukame, mafuriko na majanga mengine yanayoweza kutokana na mwelekeo wa mvua za msimu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo jijini Dodoma, Brigedia Jenerali Ndagala alisema maoni ya wadau ni muhimu ili kuimarisha mpango huo na kuwezesha Serikali kuchukua hatua sahihi za kuzuia, kupunguza madhara, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali baada ya maafa.
“Nawasihi mshiriki kikamilifu. Lazima tuwe na mpango thabiti utakaoiwezesha Serikali na wadau kuchukua hatua stahiki dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mwelekeo wa mvua za msimu,” alisema.
Alikumbusha kuwa Oktoba 17, 2025, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri wa mvua za msimu kwa kipindi cha Novemba 2025 hadi Aprili 2026, hatua iliyochochea maandalizi ya mpango huo wa dharura.

“Rasimu hii imeandaliwa kufuatia utabiri wa TMA na sasa tunaiwasilisha kwenye jukwaa hili ili mjadili na kutoa maoni kwa kuzingatia athari tarajiwa,” aliongeza.
Brigedia Jenerali Ndagala alibainisha kuwa jukwaa hilo ni muhimu katika kuweka mikakati ya pamoja ya maandalizi ya msimu, akiwataka wadau wawe na mtazamo mpana kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kupunguza athari za maafa.
Mbali na rasimu ya mpango wa dharura, alisema Ofisi ya Waziri Mkuu pia imeandaa Miongozo ya Uanzishaji na Uendeshaji wa Vituo vya Operesheni za Dharura na Timu za Kukabiliana na Dharura ngazi ya mikoa, ambayo itawasilishwa kwa majadiliano na mapendekezo ya wadau.
Kikao hicho kinalenga kuimarisha uimara wa taifa katika kukabiliana na maafa kwa kujenga mfumo madhubuti wa uratibu, maandalizi na majibu ya haraka kwa majanga yanayoweza kutokea.


