9.8 C
New York

Vyuo vikuu Urusi fursa kwa vijana Afrika

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
DIPLOMASIA ya taaluma ni eneo jingine ambalo Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imewekeza nguvu kubwa katika mahusiano yake na mataifa ya Afrika.
Kwa mwaka huu pekee, Serikali ya Urusi inayoongozwa na Rais Vladimir Putin, imetoa ufadhili wa masomo kwa vijana wa Afrika zaidi ya 5,000 waliojiunga na vyuo vikuu nchini humo.
Wakati huo huo, takwimu zinaonesha kuwa kwa miaka ya hivi karibuni, Urusi imekuwa kimbilio la Waafrika wengi linapokuja suala la kusoma elimu ya juu nje ya Bara hili.
Kwa mwaka huu, wasomi zaidi ya 40,000 waliomba ufadhili wa masomo katika Taifa hilo la Mashariki mwa Ulaya. Idadi hiyo ni mara mbili ya maombi ya mwaka jana.
Takwimu za Shirika la Diplomasia ya Utamaduni nchini Urusi, Rossotrudnichestvo, zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya maombi hayo ni kutoka Sudan, Guinea, Ghana na Chad.
Aidha, fursa ya ufadhili wa masomo imeifanya lugha ya Kirusi kuwa miongoni mwa zinazopiga hatua kubwa na kuvutia wengi kujifunza barani Afrika.
Mathalan, katika Taifa la Jamhuri ya Afrika ya Kati, Serikali ya Rais Faustin-Archange Touadera imeifanya lugha ya Kirusi kuwa somo la lazima kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Urusi inanufaika vipi?
Hata hivyo, ufadhili wa masomo unatajwa kuwa ni moja ya mikakati ya Urusi katika kuongeza ushawishi wake barani Afrika.
“Ufadhili wa masomo ni njia rahisi wanayotumia Urusi kupata washirika. Kwa sasa, Urusi inahitaji washirika,” anasema Irina Filatova, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal cha Afrika Kusini.
Vilevile, ukilinganisha na mataifa mengine ya Ulaya, gharama nafuu ya maisha na hata ada za vyuo vikuu nchini Urusi inatajwa kuwavutia wasomi wengi wanaotaka kupata elimu ya juu nje ya Afrika.
Mathalan, ada kwa kozi muhimu, ikiwamo ya afya, ni kati ya Dola za Marekani 2,000 na Dola 10,000, wakati kwa mataifa ya Ulaya na Marekani ni kati ya Dola 20,000 na Dola 40,000.
“Vyuo vikuu vya Urusi ni nafuu kuliko kusoma Ulaya na hata katika baadhi ya vyuo barani Afrika,” anasema Keith Batptis, raia wa Zimbabwe, ambaye watoto wake watatu wanasoma Urusi.
Batptis anafichua kuwa hata bei ya vyakula nchini Urusi iko chini, ukilinganisha na Zimbabwe.
Jefry Makumbe, ambaye ni raia wa Zimbabwe aliyesoma na kuhitimu Shahada ya Uandishi wa Habari wa Redio na Televisheni katika Chuo Kikuu cha Voronezh nchini Urusi, naye anasema:
“Unafuu wa maisha na uhusiano mzuri uliopo kati ya Urusi na nchi za Afrika ni sababu kubwa ya vijana wa Afrika kupenda kusoma nchini Urusi.”
Changamoto kusoma Urusi
Wakati huo huo, wapo wanaokosoa ufadhili wa masomo wa Urusi kwa wanafunzi wa Afrika wakiuita kuwa ni silaha ya kusambaza propaganda za nchi hiyo.
Pia, taasisi za kimataifa za haki za binadamu zimekuwa zikidai kuwa wanafunzi wa Afrika wanaingia Urusi kwa ufadhili wa masomo huishia kulazimishwa kujiunga na jeshi.
Ni baada ya baadhi ya wapiganaji wake waliokamatwa nchini Ukraine kukiri kuwa ni wanafunzi wa kigeni waliolazimishwa kujiunga na jeshi wakitishiwa kutupwa gerezani endapo wangekataa.
Mbali ya wanaopelekwa vitani nchini Ukraine, ripoti zinaeleza kuwa wengine wanatumikishwa katika viwanda vya kutengeneza silaha.
Filatova analizungumzia hilo alisema: “Ni mbaya sana kwa taswira ya Urusi ikiwa inafadhili masomo ya wanafunzi wa kigeni na kisha kuwatumia kwa kazi zingine.”
Historia ya ukaribu wa Urusi, Afrika
Lakini, ukaribu wa Urusi na mataifa ya Afrika, kama ilivyo kwa Asia na Latin Amerika, una historia ndefu.
Katika miaka ya 1960, maelfu ya wasomi wa Afrika, ambao wengi wao walikuja kuwa viongozi wa kupigania uhuru wa nchi zao, akiwamo Patrice Lumumba, walipata elimu zao nchini humo.
Leo hii, katika ardhi ya Mji Mkuu wa Urusi, Moscow, kipo Chuo Kikuu kilichopewa jina la Patrice Lumumba, ikiwa ni alama ya uhusiano mkubwa uliopo kati ya Urusi na Afrika.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img