Na Hassan Mwasha, Gazetini
TUMEKUWA tukiishi kwa mazoea hata katika mambo yanayoweza kuhatarisha maisha yetu. Cha kushangaza, hakuna anayejali. Tuko ‘bize’ kwa lipi wakati maisha yako hatarini? Sijui.
Leo hii, katika jamii zetu, changamoto ya afya ya akili siyo jambo linaloshitua. Ni kawaida tu kupishana na wagonjwa wa akili, kana kwamba ni watu wenye utimamu na wasio na madhara. Hakuna anayejali.
Unaweza kuwa shuhuda juu ya idadi kubwa ya watu hao huko mitaani. Wamejaa mitaani, sokoni, katika vituo vya daladala, na hata kwenye mikusanyiko mingine ya umma.
Kwa utafiti usio rasmi, kwa siku moja, ni aghalabu kutokukutana na watu wawili hadi watatu wenye changamoto ya afya ya akili. Hakuna anayeona ni hatari kwa jamii kuishi na watu wa aina hiyo katika mazingira ya kila siku. Tuko ‘bize’ na maisha!
Sisemi hivyo kwa maana ya kuhamasisha watengwe, ila haipaswi kupuuzwa kuwa watu wenye changamoto ya afya ya akili wanahitaji uangalizi maalumu.
Tujiulize; ni kwa namna gani jamii inaweza kumshitaki mtu mwenye changamoto ya afya ya akili endapo atasababisha madhara ya kujeruhi au hata kuua?
Jibu ni rahisi, kwamba hakuna namna ya kumshitaki kwa kuwa tayari jamii itakuwa imejiridhisha (kwa msaada wa madaktari) kuwa mtu huyo ana changamoto ya afya ya akili.
Mathalan, mtu mwenye changamoto ya mtandao afya ya akili amebaka, ameiba, amejeruhi au ameua. Ni kwa namna gani muhanga wa moja ya matukio hayo anaweza kupata kinga?
Ni kwa maana hiyo basi, tayari watu wenye changamoto ya afya ya akili wana kinga juu ya madhara yote watakayoisababishia jamii. Lakini, jamii haina kinga, bali inahitaji umakini tu ili kuepuka madhara yatokanayo na kundi hilo.
Kwa upande mwingine, kuachwa wakizurura mitaani pasi na mamlaka kuwawekea uangalizi maalumu inaweza kutafsiriwa kuwa ni kutolitendea haki kundi hilo la watu wenye changamoto ya afya ya akili.
Ndiyo, kwa sasa kundi hilo limeachiwa mzigo wa kujisimamia katika mahitaji yote muhimu. Ni wao kujua watakula nini, watavaa nini, watalala wapi, na hata masuala ya matibabu wanapopata maradhi.
Hapo walau unaweza kupata picha ya mazingira magumu wanayopitia, ikizingatiwa kuwa si kundi linalojihusisha na shughuli za uzalishaji, ambazo zingeweza kuwasaidia kujipatia kipato na kumudu gharama za maisha.
Kama tunavyoshuhudia kwa watoto yatima, kwanini sasa mamlaka zisione umuhimu wa jamii kuwa na vituo vingi vya kulea kundi hili la watu wenye changamoto ya afya ya akili?
Kwa kufanya hivyo, si tu itakuwa imewasaidia, bali pia itaiepusha jamii nzima na madhara mbalimbali yanayoweza kusababishwa na kundi hilo, vikiwamo vitendo vya ubakaji.
Published:


