Na Winifrida Mtoi, Gazetini
TAARIFA za uzushi zimeendelea kusambaa kwa kasi kubwa katika mitandao ya kijamii, hasa kutokana na ongezeko la watumiaji wa majukwaa hayo nchini Tanzania. Wataalamu wa mawasiliano wanaonya kuwa kusambaza taarifa zisizothibitishwa kunahatarisha amani, usalama na hata maisha ya wananchi.
Iwapo wewe ni miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, kuna hatua madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa unapokutana na taarifa zinazotia shaka. Kwanza, usisambaze. Kuzuia kuzituma kwa watu wengine ni njia ya moja kwa moja ya kuokoa maisha ya ndugu, jamaa na marafiki.
Pia ni muhimu kuripoti taarifa hizo kwa mamlaka husika ili ukweli uweze kubainishwa wazi. Vilevile, unaweza kuwasiliana na wathibitishaji habari kama Nukta Fakti ambao hutumia teknolojia na nyenzo za kidijitali kuthibitisha usahihi wa taarifa. Hatimaye, angalia vyanzo vingine vya habari ili kuhakikisha taarifa umetumia imetoka kwenye chanzo rasmi na cha kuaminika.



