*Yagusia suala la Tancoal
Na Mwandishi Wetu, Gazetini
CHEMBA ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) imetoa rai kwa Serikali kuweka sera madhubuti zitakazowawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati ya uchumi, huku ikimtaja mfanyabiashara maarufu Rostam Aziz kama mfano bora wa mwekezaji mzawa aliyefanikiwa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Septemba 23, 2025, Rais wa TCCIA, Vicent Minja, amesema kuna haja ya kuimarisha mifumo ya kisheria na sera zitakazowapa wazawa kipaumbele katika shughuli za kiuchumi, akisisitiza kuwa Watanzania wana uwezo mkubwa wa kuwekeza endapo watawezeshwa.
“Watanzania wanaweza. Ndugu Rostam Aziz ni mfano wa kuigwa, amewekeza ndani na nje ya nchi. Uwekezaji wake umechangia ajira, mapato ya kodi na ukuaji wa sekta binafsi,” amesema Minja.
Ametaja maeneo ambayo Rostam amewekeza, ikiwemo Kampuni ya Taifa Gas inayofanya kazi pia Kenya, Uganda, Zambia na Malawi, ununuzi wa hisa katika Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL), TANCOAL pamoja na mgodi wa almasi wa Petra.
Minja pia alijibu malalamiko dhidi ya mfanyabiashara Rostam Aziz kuhusu ununuzi wa hisa za Mradi wa Tanzania China International Mineral Resources Limited Coal (TANCOAL) akisema suala hilo ni sehemu ya biashara ya hisa za makampuni duniani.
“Inaweza kuwa kampuni iko hapa Tanzania lakini imesajiliwa London Stock Exchange, mimi nikatoka sasa hivi nikaenda London Stock Exchange nikatafuta wale ambao wanazile shea nataka shea za kampuni hii hapa na dau langu hili hapa nikaweka. Wakafuatwa wale ambao wanamiliki shea wakaambiwa kuna mtu anataka kununua shea zako, unataka kununua? Akikubali unanunua, ukinunua ukija huku Tanzania nimesajiliwa ile kampuni ni yangu,” amesema Minja.
Amesisitiza kuwa hatua hizo si tu kwamba zinachochea uchumi, bali pia zinaweka msingi wa ushiriki wa wazawa katika sekta nyeti na kuonesha mfano wa kizalendo katika biashara.
Aidha, amesema licha ya uwepo wa sheria kama Sheria ya Ushiriki wa Watanzania (Local Content Act), Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni za Madini za mwaka 2018, utekelezaji wake bado unahitaji kuimarishwa ili kuhakikisha Watanzania hawabaki watazamaji katika shughuli kubwa za kiuchumi.
Vilevile, ameiomba Serikali kujifunza kutoka mifano ya kimataifa kama Afrika Kusini kupitia Sera ya Uwezeshaji wa Weusi Kiuchumi (Black Economic Empowerment), na Urusi iliyoweka mfumo mpya wa usimamizi wa rasilimali baada ya enzi ya Usovieti, ili kuhakikisha Watanzania wananufaika moja kwa moja na rasilimali za taifa.


