Na Mwandishi Wetu, Gazetini
HAKAMATIKI-ndio msamiati unaoibuka kuelezea upekee wa kishindo cha mikutano ya kampeni za mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ukilinganisha na wapinzani wake waliokwisha zindua kampeni zao.
Katika siku tano pekee tangu kuzinduliwa kwa kampeni za uchaguzi zitakazodumu kwa siku 60, wachambuzi wa siasa wanasema Dk. Samia ameonyesha kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wananchi, hali iliyoakisiwa na maelfu ya watu waliofurika katika mikutano yake.
Tofauti na wapinzani wake, Dkt. Samia ameendesha mikutano 10 ya kampeni katika siku hizo tano, huku mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi akiendelea na mikutano Kanda ya Ziwa. Vyama vingine ambavyo vimezindua kampeni ni pamoja na Chaumma, CUF, AAFP, UDP na CCK, lakini kila kimoja kimefanya mikutano kati ya moja hadi miwili pekee.
Mchambuzi wa siasa na jamii, Philemon Mtoi, amesema tathmini ya siku tano zinaonyesha kuwa Dk. Samia amewashawishi wananchi wengi zaidi.
“Siku tano hizi kama ukifanya tathmini ni kweli Dk. Samia ameng’aa ukilinganisha na wagombea wengine. Hata ukisema anabeba watu, beba na wewe tuone kama watafika idadi ile,” alisema Mtoi.
Amefafanua kuwa siasa ni sanaa ya kushawishi, na kwa kuwa Dk. Samia ana uwezo wa kukusanya maelfu ya watu katika mikutano yake, hiyo ni ishara tosha ya uungwaji mkono mkubwa.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa Makame Ali amesema kufurika kwa watu kunatokana na uwezo wa chama husika, ikiwemo nguvu za kiuchumi na mtandao mpana wa chama hicho.
“Hakamatiki wala hatokamatika. Hii ni sawa na mbio za riadha, kuna wengine wanajua wanaenda tu kuongeza idadi ya washiriki. Lakini mwenye kisu kikali ndiye anakula nyama,” alisema.
Makame amekumbusha pia harambee ya kuchangisha fedha za kampeni ya CCM iliyovutia maelfu ya watu na kukusanya mabilioni ya shilingi, akisema huo ni uthibitisho wa uwezo wa chama hicho kusimamia kampeni kwa kiwango cha juu.
“Hakuna siasa bila fedha. CCM ilitafuta watu, ikachangisha, na ikapata mabilioni. Vyama vingine hata Sh milioni moja inakuwa mtihani,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa wachambuzi hao, mazingira ya kisiasa yalivyo na mtandao mpana wa CCM, ni vigumu kwa mgombea wake wa urais, Dk. Samia, kushindika kufanikisha mikutano ya kampeni yenye mvuto mkubwa kuliko wapinzani wake.


