Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Katika maadhimisho ya Siku ya Simba Duniani, taarifa mpya zinaonyesha hali ya kutisha kwani Simba, miongoni mwa wanyama mashuhuri barani Afrika, tayari wametoweka katika nchi 26 kati ya 48 zenye wanyama hao Afrika, na sasa wanapatikana katika asilimia 7 pekee ya maeneo yao ya asili.
Kupotea kwa makazi, migongano kati ya binadamu na wanyamapori, ujangili na mitego ya waya vimetajwa kama sababu kuu za kupungua kwa idadi ya simba.
Tanzania, ikiwa na idadi kubwa zaidi ya simba barani Afrika, ina nafasi ya kipekee na muhimu katika kulinda mustakabali wa mnyama huyu wa kifahari.
Ulinzi wa simba nchini si kwa manufaa ya spishi pekee, bali pia kwa usawa wa ikolojia na urithi wa kitamaduni wanaouwakilisha kote barani.
Kwa karne nyingi, simba wa Kiafrika wamekuwa ishara ya nguvu, ujasiri na uongozi, wakiwa na nafasi kubwa katika utamaduni, utambulisho na imani za kidini barani Afrika.
Shirika la Wild Africa limeonya kuhusu haja ya kuchukua hatua za haraka za kulinda simba wa porini kupitia mbinu shirikishi zinazosaidia wanyama pamoja na jamii za wenyeji.
Kwa mujibu wa Ripoti ya 2025 ya LionAid kuhusu Idadi ya Simba Afrika, idadi ya simba wa porini iko hatarini kupungua zaidi. Inakadiriwa kuwa wapo takriban simba 13,014 pekee katika Afrika Mashariki na Kusini, na simba 342 pekee Afrika Magharibi na Kati – maeneo yenye simba wa kigenetiki tofauti na walioko kwenye hatari zaidi ya kutoweka.
Takwimu tofauti kutoka Orodha ya Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasili (IUCN) ya Spishi Zilizoko Hatarini zinaonyesha kuwa idadi ya simba inaendelea kupungua. Hali ya urejeo wa spishi imetajwa kuwa “imetoweka kwa kiasi kikubwa” (Largely Depleted), ikiwa na alama ya urejeo wa asilimia 23 hadi 33 pekee.
Sababu kuu ya kupungua kwa simba ni kupotea kwa makazi yao. Zamani, simba walitanda kutoka Ulaya hadi kusini mwa Afrika, na kutoka Afrika Magharibi hadi India.
Hata hivyo, upanuzi wa makazi ya binadamu, kilimo, miundombinu na matumizi ya ardhi umepunguza makazi yao hadi asilimia 7 pekee. Kupungua kwa makazi pia kumeathiri upatikanaji wa mawindo ya asili ya simba.
Utafiti uliochapishwa hivi karibuni kwenye jarida Conservation Science and Practice umebaini kuwa mazingira yaliyopungua mawindo ni miongoni mwa vichocheo vikuu vya kupungua kwa simba. Sababu nyingine zinazotishia kutoweka kwa simba ni pamoja na migongano kati ya binadamu na wanyamapori ambapo simba huuliwa ili kulinda mifugo au kulipiza kisasi kwa vitisho vinavyodhaniwa.
Ujangili: Simba huvuliwa kwa ajili ya viungo vya miili yao kama mifupa, makucha, meno, mafuta na ngozi, vinavyotumika katika tiba za kienyeji au kuuzwa kwenye masoko haramu. Mitego ya waya: Mitego hii isiyochagua huwanasa na kuua simba, na pia hupunguza idadi ya mawindo yao.
Simba ni muhimu sana kwa afya na usawa wa mfumo wa ikolojia. Kama spishi ya msingi (keystone species), ulinzi wao huendeleza urithi wa viumbe hai – kuanzia mimea na miti hadi wanyama wanaoyategemea. Zaidi ya hayo, simba ni miongoni mwa kivutio kikuu cha watalii wa safari. Utalii wa wanyamapori unachangia asilimia 8.5 ya pato la ndani la Afrika, huku asilimia 80 ya watalii wa kimataifa wakisema wanyamapori ndio sababu kuu ya kuja barani.
Kwa kuongezeka kwa vitisho na viwango vya urejeo visivyotia moyo, kuna haja kubwa ya kuchukua hatua thabiti za uhifadhi. Mbinu shirikishi inayojumuisha kuhifadhi makazi ya asili, kushirikisha jamii, kuimarisha sheria dhidi ya uhalifu wa wanyamapori, na kuendeleza utalii endelevu inaweza kugeuza mwelekeo wa hali hii.
Umma pia una nafasi muhimu kupitia kuripoti uhalifu wa wanyamapori, kuhifadhi maeneo ya asili, na kutembelea hifadhi za taifa, ambako ada za kuingilia huunga mkono moja kwa moja kazi za walinzi na miradi ya uhifadhi.
Muda unayoyoma kwa simba wa Afrika, na maisha yao yako mikononi mwetu. Katika Siku hii ya Simba Duniani, tuchukue hatua kwa pamoja kuongeza uelewa, kuhakikisha simba wanaendelea kutembea porini, na kurudisha mngurumo wao ukisikika kote barani kwa vizazi vijavyo.


