MWANDISHI WETU, Gazetini
NI rasmi sasa, kwamba benchi la ufundi la Yanga liko chini ya kocha mpya raia wa Ufaransa, Romain Folz.
Ikielezwa kuwa amesaini mkataba wa miaka miwili, Folz ni kocha msomi, akiwa na leseni ya ukocha ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA Pro Licence).
Kuziweka sawa kumbukumbu, kocha huyo ametua Jangwani kukalia kiti cha Miloud Hamdi aliyejiunga na matajiri wa soka la Misri, Ismaily.
SOKA LA KASI, AKILI NYINGI
Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 35, ni kocha anayependa soka la kushambulia akitumia zaidi mfumo wa 4-3-3. Ni mfumo ambao Folz anataka kuona timu yake ikicheza kwa kasi, pia ikimiliki mchezo kwa kutawala eneo la kiungo.
‘CV’ YAKE IKO HIVI
Safari yake ya ukocha ilianza miaka takribani saba iliyopita, alipokabidhiwa mikoba ya kuinoa West Virginia United ya Marekani.
Lakini, alitua kwa mara ya kwanza katika soka la Afrika mwaka 2019, alipoajiriwa kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’.
Alipoondoka Uganda, alipewa nafasi hiyo ya kocha msaidizi katika benchi la ufundi la Pyramids ya Misri.
Mwaka 2020, Folz alitimkia Ghana, ambako alikuwa kocha mkuu wa Bechem United.
Baadaye, alirudi kwao, Ufaransa, alipopewa nafasi ya kuwa kocha msaidizi wa klabu ya Niort.
Mwaka 2021, Folz alirejea Afrika, safari hii akiwa kocha wa Ashanti Gold ya Ghana, kabla ya kuhamia Botswana alikoitwa na mabosi wa Township Rollers.
Mwaka 2022, kocha huyo alitua kwa mara ya kwanza katika soka la Afrika Kusini, akiajiriwa na Marumo Gallants.
Wakati huo, akawa ndiye kocha mwenye umri mdogo zaidi katika Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Kwa Afrika, pia amewahi kuzinoa AmaZulu, Horoya AC (Guinea) na Mamelodi Sundowns iliyomfuta kazi Desemba 10, mwaka jana.
KWANI YEYE ANASEMAJE?
“Najisikia Fahari kuinoa Yanga na kufanya kazi na wachezaji wenye vipaji vikubwa kama hawa, pia kuwa karibu na mashabiki wenye hamasa kama hawa.
“Lengo letu ni kuipa mafanikio makubwa klabu hii. Si tu kwenye michuano ya ndani, bali pia kuacha alama kwenye michuano ya CAF ya Ligi ya Mabingwa,” alisema Folz.
SILAHA ZAKE
Kama ilivyo kawaida, kocha mkuu huwa na jopo la wasaidizi wake. Itakuwa hivyo pia Folz ndani ya Yanga.
Yanga imeshatangaza uwepo wa kocha raia wa Tunisia, Majdi Mnasria, ambaye atawanoa makipa, akichukua nafasi ya Alae Meskini aliyejiunga na AS FAR Rabat. Mnasria amewahi kufanya kazi Tunisia, Algeria na Afrika Kusini na hivi karibuni alikuwa msaidizi wa Folz katika klabu ya Olympique Akbou ya Algeria.
Pia, Folz atakuwa na El Gawafel Sportives de Gafsa na ES Metlaoui, ambao pia ni wasaidizi wake katika klabu mbalimbali alizopita.
Published:


